• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Somalia ni mseto wa vituko na udikteta

DOUGLAS MUTUA: Somalia ni mseto wa vituko na udikteta

Na DOUGLAS MUTUA

TAIFA jirani la Somalia haliishi vituko, lakini hiki cha juzi nusra kinitegue mbavu! Kuna watu jasiri huko.

Mkuu wa polisi wa mji wa Mogadishu, Bw Saadaq Omar Hassan, alitangaza kulivunja bunge la kitaifa kwa muda ili lisijadili mswada wa kurefusha utawala wa rais wa sasa.

Afande Hassan alisema alichukua hatua hiyo peke yake ili kuwazuia wabunge kushiriki kikao cha kuvunja sheria kusudi kumfaa Rais Muhammed Abdullahi Muhammed, anayedendwa na maashiki zake ‘Farmaajo’.

Kama mzalendo wa nchi yake aliyekuwa na dhamana ya kudumisha sheria na usalama mjini Mogadishu, Afande Hassan alitangaza vikao vya bunge haramu. Kawaida yetu Waafrika hatufanyi vikao vya umma bila idhini ya polisi eti.

Hata hivyo, haukupita muda mrefu kabla ya hatua yake hiyo kumtia matatani! Kamishna wa Polisi wa nchi hiyo, Jenerali Hassan Mohamed Hijar, alimfuta kazi mara moja.

Kamishna Hijar hakumpiga kalamu tu afande wa watu, alibatilisha na uamuzi wake wa kulivunja bunge kwa muda, vikao vikaendelea na haramu iliyonuiwa kuzuiwa ikatendeka!

Mswada wenyewe ulipitishwa upesi na wabunge wote, Rais Farmaajo akaihalalisha haramu yenyewe haraka na sasa inatumika kama sheria ya nchi.

Nimeiita haramu kwa kuwa mswada wenyewe ulitiwa saini bila kupelekwa kwenye bunge la seneti ili kujadiliwa kama katiba ya nchi hiyo inavyoagiza.

Spika wa Seneti mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini humo, Bw Abdi Hashi Abdullahi, hakulifumbia jicho tendo hilo.

Aliliita ukiukaji mkubwa wa katiba ya nchi. Hii ni ithibati kwamba hatua ya Afande Hassan ina umaarufu wake nchini humo.

Hata hivyo, sasa Bw Farmaajo ataongoza taifa hilo la eneo la Upembe wa Afrika lisiloisha misukosuko kwa muda wa miaka miwili ijayo iwapo lisilotabirika halitatokea.

Tafadhali usimdhanie Afande Hassan kichaa. La hasha! Anazo akili razini kabisa, labda aliojaaliwa zaidi ya watu wengi ni ujasiri usio wa kawaida.

Hatua yake ya kulivunja bunge kwa muda ilitokana na ukweli kwamba wanasiasa wa nchi hiyo wameshindwa kukubaliana kuhusu tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Hii ina maana kwamba Bw Farmaajo ameiongoza nchi hiyo kinyume na sheria tangu mwishoni mwa mwaka jana muhula wake wa kwanza ulipofika ukingoni.

Tangu mwaka jana, wanasiasa wa Somalia wameshindwa kukubaliana kuhusu wajumbe wanaotakikana kuwachagua viongozi.

Wamekubaliana kwamba raia wasipige kura moja kwa moja kuwachagua viongozi wao; wabunge wachaguliwe na wawakilishi kisha wabunge wamchague rais, lakini jinsi ya kuwateua wawakilishi wenyewe ni kama kushuka mchongoma.

Bw Farmaajo ametumia msukosuko huo wa kikatiba kujiongezea muda wa kutawala na hataki kumwona yeyote anayethubutu kuhakiki uamuzi huo.

Natumaini Afande Hassan ataruhusiwa kusalia hai; kumfuta mtu kazi kwenye nchi kavu na maskini kama Somalia ni adhabu ya kutosha.

Nasisitiza ‘kuruhusiwa kuisalia hai’ kwa kuwa Somalia ya Farmaajo, sawa na ilivyokuwa enzi ya Muhammed Siad Barre, kuishi ndiyo bahati hasa, kufa ni kawaida.

Baada ya kuidhinisha mswada huo haramu, Bw Farmaajo amenguruma kama simba na kusema uhuru wa kujitawala wa Somalia haupaswi kuingiliwa na nchi yoyote.

Alitoa kauli hiyo kwa kuwa jamii ya kimataifa ilimuonya mapema kwamba ingemtilia vikwazo iwapo angejiongezea muda wa kutawala.

Mngurumo wa aina hiyo ni kituko cha aina yake kwa sababu Somalia ni taifa linaloishi kwa hisani ya jamii ya kimataifa. Hata mishahara ya wanasiasa wake hutoka ng’ambo.

Ni muhimu zaidi kwa Kenya na mataifa mengine ya kanda hii kutambua wana jirani jeuri asiyejali wala kubali kuhusu mwonekano wake kimataifa.

Kenya na Somalia zinazozania mpaka kwenye Bahari ya Hindi, hivyo Kenya inapaswa kumtazama jirani huyo bila kupepesa macho kwani Farmaajo ameanza kuota pembe za udikteta.

[email protected]

You can share this post!

Leicester kutegemea zaidi Maddison na Perez dhidi ya...

Mkanganyiko mkuu unavyogubika siasa za urithi Pwani