• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Patson Daka afunga mabao manne na kusaidia Leicester kupepeta Spartak Moscow katika Europa League

Patson Daka afunga mabao manne na kusaidia Leicester kupepeta Spartak Moscow katika Europa League

Na MASHIRIKA

FOWADI Patson Daka alifunga mabao manne na kusaidia Leicester City kupepeta Spartak Moscow 4-3 katika ushindi wa ugenini ulioweka hai matumaini ya masogora wa kocha Brendan Rodgers kusonga mbele katika kampeni za Europa League msimu huu.

Baada ya kukosa fursa kadhaa za kuunga kikosi cha kwanza cha Leicester msimu huu, Daka ambaye ni raia wa Zambia, alitumia mechi dhidi ya Spartak kama jukwaa zuri la kudhihirisha ukubwa wa uwezo wake uwanjani.

Mvamizi huyo mwenye umri wa miaka 23 alisajiliwa na Leicester kutoka Red Bull Salzburg ya Austria mwishoni mwa muhula uliopita wa 2020-21 kwa kima cha Sh3.4 bilioni.

Wenyeji Spartak walijiweka kifua mbele katika dakika ya 11 kupitia kwa Alexander Sobolev kabla ya mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Victor Moses kuchangia bao la pili lililojazwa kimiani na Jordan Larsson katika dakika ya 44.

Hata hivyo, Daka aliwarejesha Leicester mchezoni mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kukamilisha krosi ya Kelechi Iheanacho. Daka alikuwa pia miongoni mwa wafungaji wa mabao katika ushindi wa 4-2 uliosajiliwa na Leicester dhidi ya Manchester United katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 16, 2021 uwanjani King Power.

Alisawazisha mambo dhidi ya Spartak katika dakika ya 48 kabla ya kupachika wavuni mabao mengine ya Leicester kunako dakika za 54 na 78. Sobolev alifunga bao la tatu la Spartak dakika nne kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Leicester kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi C kwa alama nne, mbili nyuma ya viogozi Legia Warsaw ambao watamenyana na Napoli ya Italia mnamo Oktoba 21, 2021. Spartak wanakamata nafasi ya tatu kwa alama tatu, mbili zaidi kuliko Napoli wanaokokota nanga.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Chelsea waponda Malmo bila huruma kwenye soka ya UEFA ugani...

Wamiliki wa matatu wachangamkia kuondolewa kwa kafyu

T L