• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Leopards na Gor Mahia kuumizana fainali ya Betway Cup Julai 4

Leopards na Gor Mahia kuumizana fainali ya Betway Cup Julai 4

Na GEOFFREY ANENE

MIAMBA AFC Leopards na Gor Mahia watakutana katika fainali ya kipute cha Betway Cup mnamo Julai 4 baada ya kubandua wanyonge Equity Bank na Bidco United kwa njia ya penalti ugani Utalii, mtawalia.

Leopards maarufu kama Ingwe ilikuwa ya kwanza kujikatia tiketi baada ya kulemea wanabenki wa Equity 6-5 nayo Gor ikitamba 4-1 katika nusu-fainali. Ingwe ya kocha Patrick Aussems na Equity inayotiwa makali na John Baraza, zilikuwa zimetoka 0-0 katika dakika muda wa kawaida.

Isaac Kipyegon, Said Tsuma, Washington Munene, Elvis Rupia, Cylde Senaji na Hansel Ochieng’ walifunga penalti za Ingwe naye Austin Odhiambo akapoteza yake. Kipa John Oyemba wa Leopards, alipangua penalti ya Stephen Ologi, Levian Ochieng’ akapoteza yake, huku Alvin Wafula, Evans Ochieng, Derrick Ayisi, Kigaru Juma na Timothy Ngugi wakipachika zao. Hansel Ochieng’ alifungia Leopards penalti ya ushindi.

Gor ilitupa uongozi wa bao moja ikitoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida kabla ya kutamba katika upigaji wa penalti 4-2. Vijana wa kocha Vaz Pinto waliona lango kupitia frikiki safi kutoka kwa Kenneth Muguna dakika ya nne.

David Orem alisawazishia Bidco dakika ya 19 baada ya kupokea pasi ya kichwa ndani ya kisanduku na kumwaga kipa Gad Matthews. Philemon Otieno alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika za lala-salama.

Gor ilifunga penalti zake kupitia kwa Alpha Onyango, Clifton Miheso, John Macharia na Samuel Onyango. Zacharia Gathu na Orem walipoteza penalti za Bidco.Leopards na Gor zilishinda kombe hili mara ya mwisho mnamo 2017 na 2012, mtawalia. Mara ya mwisho mahasimu hawa wa tangu jadi walikutana katika fainali ya kipute hiki ni 2013 wakati Ingwe ilirarua K’Ogalo 1-0.

Zitakuwa zinakabiliana kwa mara ya 95 katika historia yao katika gozi hili maarufu kama Mashemeji Derby.Mshindi wa fainali hapo Julai 4 atatia kibindoni tuzo ya Sh2 milioni na kupata tiketi ya kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho la Afrika msimu 2021-2022.

  • Tags

You can share this post!

Uingereza wakomoa Croatia katika mechi ya kundi D kwenye...

Vijana wahimizwa kuzingatia teknolojia ya Ajira Digital...