• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Liverpool, Chelsea fataki zitafyatuka

Liverpool, Chelsea fataki zitafyatuka

NA MASHIRIKA

FATAKI zitalipuka na nyasi za uwanja wa Wembley kuumia Liverpool na Chelsea watakaposhuka dimbani hii leo kuwania ufalme wa taji la EFL Cup.

Huku Chelsea wakiwinda ubingwa wa taji hilo kwa mara ya sita, The Reds wanafukuzia rekodi ya kulinyanyua kwa mara ya tisa.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walitinga fainali baada ya kupokeza Arsenal kichapo cha jumla ya mabao 2-0 kwenye mikondo miwili ya hatua ya nne-bora mwezi Januari.

Chelsea wanaotiwa makali na kocha Thomas Tuchel walihitaji jumla ya mabao 3-0 kudengua Tottenham Hotspur kwenye kivumbi hicho.

Ingawa taji la EFL Cup haina haiba kubwa kama Kombe la Dunia ambalo Chelsea walitia kibindoni mnamo Februari 14 baada ya kukomoa Palmeiras ya Brazil 2-1, ushindi dhidi ya Liverpool utawapa motisha zaidi katika kampeni za mapambano mengine muhula huu.

Mbali na EFL Cup, Chelsea wanafukuzia pia Kombe la FA, taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye jedwali la EPL kwa alama 50 na wataendea Luton Town katika raundi ya tano ya Kombe la FA hapo Machi 2.Chelsea hawajapoteza pambano lolote kati ya mechi sita zilizopita.

Watajibwaga ugani dhidi ya Liverpool wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 2-0 dhidi ya Lille katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Jumanne ugani Stamford Bridge.

Zaidi ya kutofungwa katika mechi tatu zilizopita za EFL Cup, miamba hao wamefungwa mara mbili pekee katika michuano sita iliyopita kwenye mashindano yote.

Chelsea walizidiwa ujanja na Manchester City kwa penalti 4-3 baada ya kuambulia sare tasa mara ya mwisho walipotinga fainali ya EFL Cup mnamo Februari 2019.

Japo wanapigiwa upatu wa kutamba leo Jumapili ugani Wembley, kibarua dhidi ya Liverpool hakitakuwa chepesi ikizingatiwa fomu ya wapinzani wao walioponda Leeds United 6-0 katika mechi iliyopita ya EPL ugani Anfield.

Liverpool walinyanyua taji la EFL Cup mara ya mwisho mnamo 2011-12 walipocharaza Cardiff City 3-2 kupitia penalti baada ya sare ya 2-2 uwanjani Wembley.

Chelsea walihitaji muda wa ziada ili kukomoa Liverpool 3-2 walipokutana mara ya mwisho kwenye fainali ya EFL Cup mnamo 2004-05.

Vikosi hivyo vilisajili sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu ugani Anfield kabla ya kutoka 2-2 waliporudiana uwanjani Stamford Bridge.

Huku Chelsea wakikosa huduma za beki Ben Chilwell anayeuguza jeraha, Liverpool watakuwa bila mafowadi Roberto Firmino na Diogo Jota ambao pia wako mkekani.

  • Tags

You can share this post!

Yafichuka daraja la OKA na Azimio ni Gideon Moi

Mmiliki wa Chelsea, Abramovich, akabidhi kamati kuu...

T L