• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Real Madrid yapepeta Granada na kuendeleza presha kwa Atletico

Real Madrid yapepeta Granada na kuendeleza presha kwa Atletico

Na MASHIRIKA

REAL Madrid waliwakomoa Granada 4-1 katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Mei 13, 2021 na kuendeleza presha kwa viongozi wa jedwali Atletico Madrid.

Real ambao ni mabingwa watetezi wa taji la La Liga, sasa wanajivunia alama 78, mbili pekee nyuma ya Atletico ya kocha Diego Simeone. Zimesalia mechi mbili pekee kwa kampeni za La Liga msimu huu kutamatika rasmi.

Luka Modric aliwaweka Real kifua mbele kupitia krosi ya Miguel Gutierrez katika dakika ya 17 kabla ya Rodrygo kufunga goli la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Ingawa kiungo veteran Jorge Molina aliwarejesha Granada mchezoni katika dakika ya 71, Eden Hazard alichangia bao la tatu ambalo Real walifungiwa na Alvaro Odriozola kunako dakika ya 75, sekunde chache kabla ya Karim Benzema kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao.

Mabao mawili ya kwanza ya Real yalichangiwa na wanasoka waliozaliwa katika miaka ya 2000 – Gutierrez aliyekuwa akiwajibishwa kwa mara ya kwanza katika gozi la La Liga na Marvin Park aliyewahi kuchezea kikosi cha Tranmere Rovers nchini Uingereza.

Atletico watatawazwa wafalme wa La Liga msimu huu mnamo Mei 16, 2021 iwapo watawachabanga Osasuna nayo Real ishindwe kuangusha Athletic Bilbao.

Barcelona ambao wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 76, nne nyuma ya Atletico, watakuwa wenyeji wa Celta Vigo ugani Camp Nou.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Dortmund wacharaza RB Leipzig na kutia kapuni taji la...

Liverpool waadhibu Man-United ugani Old Trafford