• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Salah avunja rekodi ya ufungaji wa mabao ya UEFA kambini mwa Liverpool na kusaidia kikosi chake kukomoa Atletico

Salah avunja rekodi ya ufungaji wa mabao ya UEFA kambini mwa Liverpool na kusaidia kikosi chake kukomoa Atletico

Na MASHIRIKA

MOHAMED Salah aliendeleza ubabe wake ndani ya kikosi cha Liverpool msimu huu kwa kusaidia miamba hao wa soka ya Uingereza kupepeta Atletico Madrid 3-2 na hivyo kusajili ushindi wao wa tatu kutokana na mechi tatu zilizopita kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Mechi hiyo iliyochezewa uwanjani Wanda Metropolitano katika jiji la Madrid, Uhispania, lilitawaliwa na wingi wa hisia kali huku Liverpool wakiongozwa na msukumo wa kulipiza kisasi.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walifunga mabao mawili ya haraka katika kipindi cha kwanza kupitia Salah na Naby Keita kabla ya Antoine Griezmann kupachika wavuni magoli mawili na kusawazisha mambo kufikia dakika ya 34.

Griezmann aliyerejea Atletico msimu huu baada ya kuagana na Barcelona, alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 52 baada ya kumchezea visivyo fowadi wa Liverpool, Roberto Firmino.

Kuondolewa kwa Griezmann ambaye ni raia wa Ufaransa kuliwapa Liverpool fursa ya kuchuma nafuu na wakafunga bao la ushindi kupitia penalti. Penalti hiyo iliyochanjwa na Salah katika dakika ya 74 ilikuwa zao la beki Mario Hermoso kumkabili visivyo mshambuliaji Diogo Jota.

Ingawa Jota alionekana kumwangusha Jose Maria Gimenez ndani ya kijisanduku mwishoni mwa kipindi cha kwanza, refa aliwanyima Atletico mkwaju wa penalti baada ya kurejelea teknolojia ya VAR. Hatua hiyo ilimkera zaidi kocha Diego Simeone aliyeondoka uwanjani kwa hasira mwishoni mwa mchuano bila ya kumpa mkono kocha Klopp.

Salah kwa sasa ndiye mfungaji bora wa muda wote wa mabao ya UEFA kambini mwa Liverpool. Mabao mawili aliyoyafunga dhidi ya Atletico yalifikisha idadi ya magoli yake kuwa 31, moja zaidi kuliko nahodha wa zamani wa Liverpool, Steven Gerrard ambaye sasa ni kocha wa Rangers ya Ligi Kuu ya Scotland.

Liverpool kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kutokana na 21 zilizopita kwenye mashindano yote. Kikosi hicho kimepachika wavuni mabao 30 kutokana na mechi tisa zilizopita na kimefunga wastani wa mabao matatu katika kila mojawapo ya mechi saba zilizopita ugenini msimu huu.

Masogora wa Klopp kwa sasa wanadhibiti kilele cha Kundi B kwa alama tisa, tano zaidi kuliko nambari mbili Atletico ambao wana pointi sawa na FC Porto ya Ureno iliyopepeta AC Milan 1-0 katika mchuano mwingine wa Jumanne usiku.

Ilikuwa katika uwanja wa Wanda Metropolitano ambapo Liverpool walikung’uta Tottenham Hotspur kwenye fainali ya UEFA mnamo 2019 na kunyanyua ufalme wa kipute hicho. Hata hivyo, walipigwa 1-0 na Atletico katika uga uo huo kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa kipute hicho msimu uliofuata wa 2020.

Mbali na kuendeleza ubabe wao, Liverpool walikuwa na kiu ya kulipiza kisasi dhidi ya Atletico waliowadengua kwenye hatua ya 16-bora ya kivumbi hicho muhula uliopita wa 2020-21 kwa jumla ya mabao 4-2. Ari ya Liverpool ilichangiwa zaidi na ushindi mnono wa 5-0 waliosajili dhidi ya Watford katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Jumamosi iliyopita ugani Vicarage Road.

Liverpool walifungua kampeni za UEFA muhula kwa kutandika AC Milan 3-2 mnamo Septemba 15. Walishuka dimbani kwa pambano dhidi ya Atletico wakiwa na motisha tele baada ya kucharaza FC Porto ya Ureno 5-1 katika mechi ya awali kwenye kipute hicho.

Liverpool na Bayern Munich ndizo timu za pekee zinazojivunia idadi kubwa zaidi ya mabao kutokana na mechi za kwanza za UEFA muhula huu.

Chini ya mkufunzi Julian Nagelsmann, Bayern walipiga Barcelona 3-0 mnamo Septemba 14 kabla ya kuponda Dynamo Kyiv ya Ukraine 5-0 wiki mbili zilizofuata.

Miamba hao wa soka ya Ujerumani watakuwa wageni wa Benfica hii leo nchini Ureno katika mechi ya Kundi E.

Atletico waliambulia sare tasa dhidi ya Porto katika mchuano wa kwanza wa UEFA msimu huu kabla ya kuwapepeta Milan 2-1 katika mechi iliyofuata. Milan wanavuta mkia bila pointi yoyote baada ya kupoteza mechi zote tatu zilizopita kundini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Man-City wang’aria Club Brugge huku chipukizi Cole...

‘Deep State’ ilivyozima mashujaa

T L