• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Makinda wa Nakuru walenga kuchezea Harambee Stars

Makinda wa Nakuru walenga kuchezea Harambee Stars

NA RICHARD MAOSI

TIMU ya Nakuru Youth Sports Association(NYSA) U-10 inashirikisha wachezaji wachanga, wenye mapenzi ya dhati katika ulingo wa soka, kutoka mitaa ya Freehold, Langalanga, Kasarani na St Marys .

Baadhi yao wanatokea kwenye mitaa ya mabanda na familia zenye kipato cha chini, ila kupitia kabumbu wamefanikiwa kuunganika kwenye jumuia ya wanamichezo wakiamini kuwa watakuja kufika mbali..

Wengi wao wakiwa ni wanafunzi katika shule za msingi, wameimarisha makali na kuingia katika ligi za watoto katika kaunti ya Nakuru kutokana na juhudi zao za kutandaza soka safi.

Wachezaji hawa hufanyia mazoezi yao kila siku ya Jumamosi na Jumapili, katika uwanja wa Afraha na wakati mwingine wao hushiriki mechi za nyumbani kwenye uwanja wa Nakuru Athletics Club(NAC).

Mkufunzi mkuu Dickson Gitari anasema alianzisha kikosi hiki yapata miaka miwili iliyopita akilenga kutoa fursa kwa wachezaji chipukizi kukuza talanta zao.

Aidha alilenga kuwashughulisha wanafunzi, hususan wakati wa likizo ndefu kila mwaka wasije wakajiingiza kwenye mihadarati wala utovu wa nidhamu.

Gitari anasema msimu mrefu wa janga la corona baina ya Machi mpaka Disemba 2020 alikuwa na wakati wa kutosha kunoa zana mahiri, ambazo anaamini kuwa siku moja wengi wao watakuja kuchezea timu ya taifa Harambe Stars.

“Soka ya watoto imekuwa ikipuziliwa mbali, mara nyingi wazazi wakiwanyima watoto wao nafasi ya kushiriki kwenye michezo labda kutokana na kasumba ya zamani , kuwa soka sio ya maana”akasema.

Gitari anasema kuwa soka inaweza kumfanya mchezaji aje kuwa mtu wa maana katika jamii kwa mfano Victor Wanyama na Michael Olung’a ambao wanasakata soka ya kulipwa Kimataifa.

Hata hivyo Gitari anasema kuwa ni wakati jamii na sekta mbalimbali , kujitokeza ili kufadhili michezo hasa kandanda ili kuwapatia wachezaji wa kesho matumaini, mbali na kutangaza bidhaa zao.

Ikumbukwe kuwa timu nyingi za mitaani zimekuwa zikijigharamia wakati wa safari za mechi za ugenini, gharama ambayo imekuwa ikisukumiwa wazazi au timu.

Anaona kuwa miundo misingi bora, mechi nyingi za kupimana nguvu, motisha kwa wachezaji, mazoezi ya kutosha na uongozi bora katika soka ndiyo mambo ya kimsingi kupaisha soka kwa timu za mitaani ambazo zinategemea wahisani.

Kinyume na siku za mbeleni wachezaji, hawakuwa wakitiliwa maanani labda ndio sababu baadhi yao waliwakilisha taifa lakini wakaishia kufa wakiwa mafukara.

Aidha anaongezea kuwa ni vyema kwa mchezaji kuangazia kipaji chake akiwa mdogo ali aboreshe taaluma yake ya soka kadri ya muda.

Mbali na kuwa na timu ya watoto Gitari ana timu ya akina dada na msururu wa timu za wanaume U-10,U-13,U16,U-20 na timu ya wazee.

Alieleza Taifa Leo kuwa kadri ukarabati wa Afraha Stadium unapoendelea kiwango cha soka kitakuja kuimarika mbeleni kwani mechi nyingi za kimataifa zitakuwa zikichezwa Nakuru.

  • Tags

You can share this post!

Nakuru West Queens washinda Eldoret Falcons 3-2 ugenini

Harambee Stars yakata kidomo cha Watanzania