• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:16 PM
Mambo yalivyokuwa katika dirisha la uhamisho kwa Wakenya ughaibuni

Mambo yalivyokuwa katika dirisha la uhamisho kwa Wakenya ughaibuni

Na GEOFFREY ANENE

Wanakabumbu Wakenya ughaibuni walikuwa na shughuli nyingi kutafuta makao mapya katika kipindi cha uhamisho cha Januari 2021. Hii hapa taarifa jinsi mambo yalivyokuwa kwa Wakenya sokoni katika mwezi huo.

Michael “Engineer” Olunga

Mshindi wa Kiatu cha Dhahabu na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Japan (J1 League) mwaka 2020 Olunga alikuwa jina kubwa kabisa kutoka Kenya aliyehama Januari.

Baada ya miaka miwili na nusu katika klabu ya Kashiwa Reysol, Olunga alielekea nchini Qatar kujiunga na Al Duhail SC kwa kandarasi ya miaka mitatu mnamo Januari 12. Al Duhail ilimwaga Sh800 milioni (Yuro milioni sita) kupata huduma za Olunga. Mshambuliaji huyu maarufu kama Engineer pia ndiye jina kubwa kuhama J1 League mwezi Januari.

Olunga amefungia waajiri wake wapya mabao matatu, yote yakipatikana katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Al Ahli Doha kwenye kipute cha Amir Cup. Alikuwa ameanza maisha na mabingwa hao wa Qatar bila bao katika mechi za ligi dhidi ya Al Sadd na Qatar SC.

Wakenya wengi waligawanyika kuhusu kuhamia kwake Qatar. Wakosoaji wake walitaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ahamie Bara Ulaya wakidai kuwa ligi ya Qatar ni ya wachezaji wanaoelekea kustaafu.

Waliomuunga mkono hawakujali anahamia ligi gani muradi tu mchezaji huyo wa zamani wa Gor Mahia apate donge nono kuliko fedha alizokuwa akipokea Kashiwa.

Johanna Omolo

Baada ya kuwa nchini Ubelgiji tangu mwaka 2007, Omolo,31, alifanya uhamisho wa kushangaza alipojiunga na timu inayoshiriki Lig Kuu ya Uturuki ya Buyuksehir Belediye Erzurumspor mnamo Januari 14.

Aliondoka Cercle Brugge inayochechemea kuwa na timu hiyo inayokodolea macho kuangukiwa na shoka, kwa ada inayosalia siri. Kandarasi mpya ya kiungo huyo mkabaji itakatika Juni 30.

Omolo ameanza maisha vyema nchini Uturuki akishirikishwa katika michuano mitatu iliyopita ambayo Erzurumspor imezoa alama saba kati ya tisa dhidi ya Kasimpasa, Alanyaspor na Ankaragucu na inakaribia kujiondoa kutoka mduara hatari wa kutemwa katika nafasi ya 18 kwenye ligi hiyo ya klabu 21.

Henry Ochieng’

Kiungo huyo wa kati ambaye ni mzawa wa jiji la London, alivuka mpaka kutoka Jamhuri ya Ireland na kujiunga na timu ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 ya Watford kutoka Cork City mnamo Januari 25.

Alisaini kandarasi ya miezi sita akitokea Cork bila ada ya uhamisho. Ochieng’,22, ambaye ameitwa katika timu ya taifa ya Harambee Stars mara moja, alikuwa ameng’ara msimu uliopita akiwa Cork City kiasi cha kuvutia timu hiyo kutoka Ligi ya Daraja yaPili Uingereza. Alihama Cork City iliyotemwa kutoka Ligi Kuu Ireland.

Ismael Dunga

Nyota Michael Olunga aliacha pengo kubwa linalofaa kujazwa kwenye J1 League baada ya kufuma wavuni mabao 28 akiibuka mfungaji bora na mchezaji bora nchini Japan 2020.

Baada ya Olunga kuondoka, J1 League ilipata Mkenya mwingine Dunga. Mshambuliaji huyu mwenye umri wa miaka 27 ni mali ya Sagan Tosu.

Alitokea nchini Albanian katika klabu ya Vllaznia inayoongoza Ligi Kuu katika taifa hilo la Bara Ulaya. Sagan ililipa Sh9.3 milioni (Yuro 70,000) kupata huduma za Dunga mnamo Januari 25.

Dunga atagonga umri wa miaka 28 mnamo Februari 24, siku mbili kabla ya Ligi Kuu ya Japan ya msimu mpya ianze. Kandarasi yake na Sagan Tosu itatamatika Januari 31, 2022.

Masoud Juma

Mshambuliaji huyu ni mchezaji wa Difaa Hassani El Jadidi (DHJ). Masoud ama Masud anavyofahamika, alijiunga na klabu hiyo inayoshriki Ligi Kuu ya Morocco mnamo Januari 25 bila ada ya uhamisho.

Juma, ambaye anasherehekea kufikisha umri wa miaka 25 hapo Februari 3, aliingia DHJ baada ya kuwa na JS Kabylie inayoshiriki Ligi Kuu Algeria kwa karibu mwaka mmoja na nusu.

Pistone Mutamba

Mvamizi huyu mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na Asswehly SC kwenye Ligi Kuu ya Libya mnamo Januaryi 26.

Alilazimisha uhamisho wake kutoka Bidco United inayoshiriki Ligi Kuu Kenya akiwa amesalia na miezi miwili katika kandarasi yake. Asswehly ni klabu ya kwanza ya kigeni ya mchezaji huyo wa zamani wa Wazito na Sofapaka.

David Odhiambo Owino

Calabar anavyofahamika kwa jina la utani, aliondoka Zesco United na kujiunga na klabu nyingine kwenye Ligi Kuu Zambia Napsa Stars mnamo Januari 9 bila ada ya uhamisho.

Beki huyu wa kati mwenye umri wa miaka 32, alikuwa amesakatia Zesco tangu Januari 1, 2015.

Alikuwa mmoja wa wachezaji wanne kutoka Kenya waliokuwa Zesco pamoja na washambuliaji Jesse Were na John Makwata na kipa Ian Otieno.

Calabar amejiunga na Napsa Stars kwa kandarasi ya miaka miwili. Napsa Stars pia ina kipa Mkenya Shaban Odhoji.

John Avire

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Kakamega Homeboyz, Nakumatt, Bandari na Sofapaka alinyakuliwa na Aswan FC kutoka Tanta FC iliyotemewa kutoka Ligi Kuu ya Misri msimu uliopita.

Alitua Aswan Desemba 6, 2020. Avire, 23, alianza maisha vyema katika klabu ya Aswan, akishinda mechi mbili za kwanza, lakini mambo yamegeuka na kuwa magumu.

Aswan haijaonja ushindi katika michuano saba mfululizo na kuporomoka kutoka juu ya jedwali hadi nambari 12 kwenye ligi hiyo ya klabu 18.

Harun Shakava

Beki huyu wa kati amejiunga na Gor Mahia baada ya kuondoka Nkana inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia juma moja lililopita.

Ameajiriwa na mabingwa hao wa Kenya kwa kandarasi ya miaka miwili. Huku Wakenya wengi wakipata makao, winga wa zamani wa Beijing Renhe nchini Uchina Ayub Timbe na aliyekuwa mshambuliaji wa FC Masr nchini Misri Cliff Nyakeya badowanasalia bila klabu.

Naye mshambuliaji Timothy Otieno, ambaye alijiunga na Napsa Stars mnamo Novemba 1, 2020 kutoka Tusker FC, amerejea nyumbani kuwajibikia ‘Batoto ba Mungu’ Sofapaka.

You can share this post!

Wakenya njaa viongozi wakipiga domo

Siaya kaunti ya kwanza kupitisha BBI