• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 9:50 AM
Man-City na Borussia Dortmund waingia 16-bora UEFA licha ya kuambulia sare tasa nchini Ujerumani

Man-City na Borussia Dortmund waingia 16-bora UEFA licha ya kuambulia sare tasa nchini Ujerumani

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola amekiri kuwa kikosi chake cha Manchester City kina tatizo kubwa la kuchanja mikwaju ya penalti licha ya sare tasa dhidi ya Borussia Dortmund nchini Ujerumani kuwakatia tiketi ya hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Riyad Mahrez aliyechezewa vibaya na Emre Can ndani ya kijisanduku alishindwa kufunga penalti baada ya kombora lake kupanguliwa na kipa Gregor Kobel.

Matokeo hayo ugani Signal Iduna Park yaliwezesha pia Dortmund kutinga hatua ya 16-bora.

“Tangu nianze kudhibiti mikoba ya Man-City mnamo 2016-17, tumepoteza jumla ya penalti 25 na nyingi za penalti hizo zimekuwa katika michuano ya UEFA,” akasema Guardiola.

Man-City wanajivunia kufunga jumla ya penalti 12 kati ya 17 kwenye UEFA na 36 kati ya 52 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika historia yao.

Kufikia sasa, Mahrez amepoteza penalti tatu kati ya nne zilizopita akivalia jezi za Man-City baada ya kufunga tisa kati ya 10 za kwanza.

Guardiola alimwondoa uwanjani mvamizi wake tegemeo, Erling Haaland mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya nyota huyo raia wa Norway kugusa mpira mra 13 pekee. Alikiri baadaye kuwa sogora huyo wa zamani wa Dortmund alikuwa na homa na jeraha dogo la mguu.

Dortmund walipoteza nafasi nyingi za wazi kupitia kwa chipukizi Youssoufa Moukoko, 17, aliyemtatiza pakubwa kipa Stefan Ortega aliyekuwa akidakia Man-City kwa mara ya kwanza.

Japo Man-City wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA wakisalia na mechi moja zaidi, miamba hao wameshinda mechi moja pekee kati ya nne zilizopita katika mashindano yote. Waliambulia sare tasa dhidi ya Copenhagen ya Denmark katika UEFA kabla ya Liverpool kuwakomoa 1-0 ligini. Walitandika Brighton 3-1 katika EPL mnamo Oktoba 22, 2022 kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Dortmund.

MATOKEO YA UEFA (Jumanne):

RB Salzburg 1-2 Chelsea

Celtic 1-1 Shakhtar Donetsk

RB Leipzig 3-2 Real Madrid

Dortmund 0-0 Man-City

PSG 7-2 Maccabi Haifa

Sevilla 3-0 FC Copenhagen

Dinamo Zagreb 0-4 AC Milan

Benfica 4-3 Juventus

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mawaziri watumikie wananchi wote bila kuegemea...

Barcelona washuka hadi ligi ndogo ya Europa League baada ya...

T L