• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:47 PM
TAHARIRI: Mawaziri watumikie wananchi wote bila kuegemea mirengo

TAHARIRI: Mawaziri watumikie wananchi wote bila kuegemea mirengo

NA MHARIRI

BAADA ya Bunge kuidhinisha mawaziri wote 24 waliopendekezwa na Rais William Ruto, sasa kilichosalia ni kuanza kutekeleza majukumu yao.

Kuidhinishwa kwa mawaziri hawa kumejiri huku kukiwa na manung’uniko, kutoka huko huko bungeni na hata nje ye bunge.

Kamati iliyowapiga msasa mawaziri hao iligawika mapande mawili kuwahusu wawili wao, na ikakubaliana na kauli moja kwamba mmoja hakustahili kupitishwa.

Wabunge wa Azimio waliokuwa kwenye kamati hiyo, walikataa kuteuliwa kwa mawaziri Aisha Jumwa (Utumishi wa Umma) na Mithika Linturi (Kilimo na Ustawi wa Mifugo).

Kwenye ripoti yao, walisema kwamba wawili hao wangali na kesi mahakamani. Bi Jumwa ana kesi iliyoahirishwa jana Jumatano na Mahakama Kuu ya Mombasa, kuhusiana na mauaji ya mkazi wa Malindi.

Naye Bw Linturi hata baada ya kuondolewa kesi ya madai ya kutaka kujaribu kubaka, alikiri kuwa angali na kesi 35.

Hapa Kenya, sheria inasema mtuhumiwa hana hatia hadi mahakama iamue hivyo. Kwa msingi huo, mrengo wa Kenya Kwanza kwenye kamati ulidai kuwa kwa vile hawajapatikana na hatia, wanastahili kuidhinishwa.

Suala walilosahau wabunge ni kwamba, uamuzi wa jaji Mumbi Ngugi umekuwa ukitumika, kwamba mtu anayetuhumiwa anapaswa kukaa kando hadi kesi yake iamuliwe.

Ni uamuzi huo uliowang’oa ofisini magavana Moses Lenolkulal wa Samburu, Mike Sonko (Nairobi), Ferdinand Waititu ‘Baba Yao’ (Kiambu) na aliyekuwa waziri wa Fedha, Henry Rotich.

Kuna tofauti gani ya kesi zilizowakabili maafisa hao na mawaziri hawa wawili?

Pia kuna Bi Penina Malonza ambaye aliokolea na wabunge baada ya wanakamati kusema hakuwa amefuzu kwenye mahojiano.

Kauli ya wabunge kuwa kwenye mtihani mtu anaweza kuanguka kwa sababu mbalimbali, haifai kuingizwa katika suala hili.

Lengo la kuwahoji watu wanaotaka kazi, ni kuwachuja na kuajiri wale wanaostahili.

Kinyume chake, bunge letu limegeuza shughuli ya kupiga msasa kuwa utekelezaji tu wa hitaji la kikatiba.

Hivyo basi, kwa kuwa mawaziri hao wameidhinishwa hata baada ya kuwa na dosari, wanapoapishwa wajue kuwa Wakenya watakuwa wakiwamulika kwa karibu.

Ni juu yao kudhihirishia ulimwengu kuwa dosari hizo ni mambo yaliyopita.

Ofisi wanazochukua ni za umma. Wameingizwa hapo kwa niaba ya umma na wala si ofisi zao kama watu wanavyotaka kuamini.

Ni sharti mawaziri hao wafahamu kwamba, hata kama waliteuliwa kwa sababu ya kumfanyia kampeni Dkt Ruto, kuna maelfu ya wenzao waliofanya kampeni na pengine kutumia raslimali nyingi kuwashinda.

Wachape kazi kwa niaba ya Wakenya wote kwa sababu wao sasa ni mawaziri wan chi, si mirengo au kwao wanakotoka.

You can share this post!

Uhuru ashiriki juhudi za kuleta amani Ethiopia

Man-City na Borussia Dortmund waingia 16-bora UEFA licha ya...

T L