• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Man-City waingia robo-fainali za UEFA licha ya Sporting Lisbon kuwalazimishia sare tasa ugani Etihad

Man-City waingia robo-fainali za UEFA licha ya Sporting Lisbon kuwalazimishia sare tasa ugani Etihad

NA MASHIRIKA

MANCHESTER City walitinga robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu licha ya Sporting Lisbon ya Ureno kuwalazimishia sare tasa katika mchuano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora mnamo Jumatano usiku ugani Etihad.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walifuzu kwa raundi hiyo ya nane-bora kwa jumla ya mabao 5-0 waliyojivunia ugenini kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Februari 15, 2022.

Japo walitarajiwa kushambulia, Sporting waliibana sana ngome yao katika vipindi vyote viwili vya mchezo huku wakionekana kuhofia kufungwa mabao zaidi jinsi hali ilivyokuwa katika pambano la mkondo wa kwanza.

Raheem Sterling na Phil Foden walipoteza nafasi kadhaa za kuweka Man-City kifua mbele katika kipindi cha kwanza baada ya fataki zao kudhibiti vilivyo na kipa Antonio Adan.

Ingawa Gabriel Jesus alicheka na nyavu za wageni wao mwanzoni mwa kipindi cha pili, bao lake halikuhesabiwa baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alikuwa ameotea alipopokezwa krosi na Riyad Mahrez.

Man-City walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakifahamu kwamba walikuwa tayari wamefanya kazi kubwa katika mkondo wa kwanza ugenini. Hilo lilidhihirishwa na maamuzi ya Guardiola kumpanga michumani kipa chaguo la tatu, Scott Carson aliyechukua nafasi ya mlinda-lango tegemeo, Ederson Moraes.

Carson, 36, alikuwa akiwajibikia Man-City kwa mara ya kwanza msimu huu na alijituma vilivyo mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kwa kupangua kombora aliloelekezewa na Paulinho Fernandes.

Hii ni mara ya tano mfululizo kwa Man-City kufuzu kwa robo-fainali za UEFA na watasubiri hadi Machi 18, 2022 kufahamu mpinzani wao katika hatua hiyo ya nane-bora.

Ilikuwa pia mara ya kwanza tangu mwishoni mwa Oktoba 2021 kwa Man-City kukamilisha mchuano wa pambano lolote katika uwanja wao wa nyumbani bila kufunga bao.

Mechi hiyo dhidi ya Sporting ilikuwa ya 100 kwa kiungo mkabaji wa Man-City, Fernandinho Luiz Rosa kunogesha katika historia ya kipute cha UEFA. Man-City wanafukuzia mataji matatu msimu huu likiwemo Kombe la FA na ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambao wanapigiwa upatu wa kuuhifadhi.

Kufikia sasa, wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 69 kutokana na mechi 28. Mgongo wao unasomwa kwa karibu na Liverpool ambao wamejizolea pointi 63 kutokana na michuano 27. Baada ya kuvaana na Crystal Palace ligini mnamo Machi 14, Man-City wameratibiwa kumenyana na Southampton kwenye robo-fainali za Kombe la FA kabla ya kurejelea kampeni za EPL dhidi ya Burnley, Liverpool na Wolves kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

UCHAMBUZI WA FASIHI: Jinsi ya kujibu Maswali kuhusu...

Kenya Kwanza wapiga abautani kuhusu mtaala

T L