• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Man U waenda kichinjioni Newcastle huku Arsenal wakialika mbwamwitu Emirates

Man U waenda kichinjioni Newcastle huku Arsenal wakialika mbwamwitu Emirates

NEWCASTLE, Uingereza

NEWCASTLE, Uingereza: Manchester United wanarejea ‘kichinjioni’ ugani St James’ Park kutafuta pointi dhidi ya Newcastle ligini leo baada ya wote kupata masikitiko kwenye Klabu Bingwa Ulaya katikati mwa wiki.

United (nambari sita) walitupa uongozi wa 2-0 wakitoka 3-3 dhidi ya Galatasaray nchini Uturuki na wananing’inia pabaya katika mashindano hayo ya Ulaya.

Newcastle ya kocha Eddie Howe (nambari saba) pia ilidondosha alama muhimu katika sare ya 1-1 dhidi ya Paris Saint-Germain baada ya Kylian Mbappe kusawazisha kupitia penalti ya utata dakika ya mwisho.

Vijana wa kocha Erik ten Hag walipoteza 2-0 ligini kupitia mabao ya Joe Willock na Callum Wilson mwezi Aprili ugani St James’ Park. Pia, walisalimu amri 3-0 uwanjani Old Trafford mwezi uliopita kwenye Kombe la Carabao baada ya kufungwa na Miguel Almiron, Lewis Hall na Willock.

Mvamizi Marcus Rashford anarejea katika kikosi cha United baada ya kukosa ziara ya Galatasaray akitumikia marufuku ya kadi. Yuko huru kwa mashindano ya Uingereza. Licha ya masihara, kipa Andre Onana anatarajiwa kuendelea kudakia United.

Newcastle imo mbioni kukaribisha Sean Longstaff baada ya kupona jeraha la kifundo. Hata hivyo, Newcastle, ambayo itategemea mshambulizi Alexander Isak na ni moja ya klabu na rekodi nzuri nyumbani, bado itakosa huduma za tegemeo kadhaa wakiwemo Wilson na Willock.

Viongozi Arsenal wana fursa nzuri ya kuongeza mwanya juu ya jedwali hadi pointi nne wakizidia maarifa nambari 12 Wolves ugani Emirates.

Mjerumani Kai Havertz amefungia Arsenal katika mechi mbili mfululizo na huenda ndiye atakuwa tofauti kati ya timu hizi mbili.

Vijana wa kocha Mikel Arteta wanaofukuzia ushindi wa tano mfululizo msimu huu, wamelemea Wolves mara nne mfululizo kwa jumla ya mabao 10-1.

Watatumai kuendeleza ukatili huo pia wakiwategemea Bukayo Saka na Declan Rice. Wolves walipoteza 3-2 dhidi ya Fulham Jumatatu. Wamepata ushindi mmoja katika michuano minne iliyopita. Wolves wanajivunia wachezaji matata kama Hwang Hee-Chan na Craig Dawson anayerejea kikosini baada ya kutumikia marufuku ya kadi.

RATIBA EPL (Uingereza):Desemba 2 – Brentford v Luton Town (6.00pm), Arsenal v Wolves (6.00pm), Burnley v Sheffield United (6.00pm), Nottingham Forest v Everton (8.30pm), Newcastle v Manchester United (11.00pm); Desemba 3 – Chelsea v Brighton & Hove Albion (5.00pm), Liverpool v Fulham (5.00pm), West Ham v Crystal Palace (5.00pm), Bournemouth v Aston Villa (5.00pm), Manchester City v Tottenham Hotspur (7.30pm)

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri Paul Mackenzie sasa asukumwa jela mwaka mzima

Sherehe za utamaduni zanoga mji wa kale wa Lamu usalama...

T L