• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mhubiri Paul Mackenzie sasa asukumwa jela mwaka mzima

Mhubiri Paul Mackenzie sasa asukumwa jela mwaka mzima

NA ALEX KALAMA

Mhubiri tatanishi Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International mnamo Ijumaa amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja bila faini, baada ya kupatikana na hatia ya kutumia filamu ambazo hazijaidhinishwa na bodi ya filamu nchini, kuendesha mahubiri yake kanisani.

Filamu hizo zinasemekana kuchochea watoto kususia masomo, na hata wazazi kugoma kuwapeleka wana wao shuleni.

Mahakama ya Malindi ilimkuta na hatia ya kukiuka sheria za uainishaji na usambazaji wa filamu.

Mackenzie mwezi uliopita alipatikana na hatia ya shtaka la kumiliki na kusambaza filamu kwa umma ambazo hazijachunguzwa na kuainishwa na Bodi ya Uainishaji wa Filamu nchini (KFCB) kinyume na kifungu cha 12 cha Sheria ya Filamu na Jukwaa kwa kuendesha filamu na studio bila leseni.

Awali, Hakimu Mkazi wa Malindi Onalo Olga alikuwa amesema upande wa mashtaka ulithibitisha bila shaka yoyote mashtaka mawili ya kumiliki filamu ambazo hazijaainishwa, na kuendesha studio ya kurekodia filamu bila leseni zaidi ya shaka.

“Mshukiwa amepatikana na hatia kwa mashtaka mawili ya kumiliki na kusambaza filamu kwa umma ambazo hazijachunguzwa na kuainishwa na Bodi ya Uainishaji wa Filamu Nchini (KFCB) na kuendesha studio ya kurekodi filamu na kutengeneza filamu bila leseni halali,” alisema hakimu.

Hakimu huyo hata hivyo alimuachiliaa huru Mackenzie katika shtaka la kwanza ambapo alishtakiwa kwa kuchochea umma kukiuka sheria.

Hapa, serikali ilidai kuwa Mackenzie alichochea watoto dhidi ya kuhudhuria shule na kutumia zaidi filamu hizo kuwachochea watu dhidi ya Wahindu, Wabudha, na Waislamu.

“Upande wa mashtaka haujathibitisha shtaka hilo kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, hivyo basi mshukiwa ameachiliwa kwa kosa la kwanza la uchochezi wa uvunjaji wa sheria,” alisema hakimu huyo.

Mackenzie alikuwa amejitetea kwamba hajawahi kusababisha migogoro kati ya dini kupitia mahubiri yake, ambayo alisema yalilenga ujumbe wa nyakati za mwisho kwa wafuasi wake na wale waliojali kusikiliza.

“Yaliyomo katika kanda ya DVD yalikuwa maudhui ya wachungaji na makanisa mbalimbali duniani kote. Nilikuwa na kituo cha runinga cha Kanisa la Good News International Church lakini upande wa mashtaka haukuleta ushahidi kuonyesha kuwa vidio zilizofikishwa mahakamani zilipeperushwa na kituo cha runinga cha Times,” alisema.

Mackenzie aliiambia mahakama kuwa anafahamu kuwa jumbe zake za nyakati za mwisho ziko kwenye chaneli ya YouTube inayoitwa Times Tv na kwamba yeye ndiye alizipakia huko ili kuwasilisha mafundisho yake.

Hata hivyo, mahakama ilisema kuwa serikali kupitia kwa Kiongozi wa Mashtaka Joseph Mwangi ilithibitisha kesi dhidi ya Mackenzie bila shaka yoyote.

Hakimu alibaini kuwa Mackenzie alishindwa kujiondoa kutoka kwa ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa mashtaka na vielelezo vikiwemo kanda za video akitoa mahubiri hayo makali.

Pia, mahakama iliona kuwa Mackenzie alikiri kuwa Televisheni ya Times ilikuwa ya kanisa lake, ambapo filamu za DVD zenye mahubiri ya wakati wa mwisho zilipatikana ofisini kwake.

Akitoa huku mnamo Ijumaa, Hakimu Onalo alisema mhubiri atatumikia kifungo cha miezi 12 gerezani bila faini.

Inadaiwa kuwa Mackenzie alirekodi filamu hizo kati ya Januari na Aprili 2019 katika kanisa lake lililoko eneo la Furunzi mjini Malindi.

  • Tags

You can share this post!

Israel yaanza tena kulipua Gaza muda wa kusitisha mapigano...

Man U waenda kichinjioni Newcastle huku Arsenal wakialika...

T L