• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Man-United waajiri kocha Erik ten Hag kwa mkataba wa miaka mitatu

Man-United waajiri kocha Erik ten Hag kwa mkataba wa miaka mitatu

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamemteua kocha Erik ten Hag wa Ajax kuwa mkufunzi wao mpya.

Mholanzi huyo mwenye umri wa miaka 52 atatwaa mikoba ya Man-United kutoka kwa kocha mshikilizi Ralf Rangnick kwa mkataba wa miaka mitatu mwishoni mwa msimu huu. Ataongezewa mwaka mmoja zaidi kwenye kandarasi yake kutegemea matokeo ya kikosi hicho chini yake.

Rangnick, aliyejaza pengo la Ole Gunnar Solskjaer aliyetimuliwa mnamo Novemba 2021 kutokana na matokeo duni.

Ten Hag atakuwa kocha wa tano kuajiriwa na Man-United kwa mkataba wa kudumu tangu mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kuagana na Sir Alex Ferguson aliyestaafu mnamo 2013.

“Ni tija na fahari tele kuteuliwa kuwa kocha wa Man-United. Ninatazamia makuu zaidi kadri ninavyojiandaa kwa changamoto mpya ya kudhibiti mikoba ya kikosi hiki maarufu,” akasema Ten Hag.

“Ninajua historia ya klabu hii na utashi wa mashabiki wao. Kubwa zaidi katika maazimio yangu ni kuanza kushindia kikosi hiki mataji na kuwapa ufanisi wanaostahili,” akaongeza kocha huyo.

Kufikia sasa, Man-United wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 54, tatu zaidi nyuma ya Tottenham Hotspur wanaofunga orodha ya nne-bora ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2022-23. Zimesalia mechi tano pekee kabla ya kampeni za EPL kutamatika rasmi.

Kwa upande wao, Ajax wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) na pengo la alama nne linawatenganisha na nambari mbili PSV Eindhoven waliokomoa kwenye fainali ya Dutch Cup mnamo Aprili 17, 2022. Zimesalia pia mechi tano kwa kipute cha Eredivisie kutamatika rasmi.

Ten Hag alitwaa mikoba ya Ajax mnamo Disemba 2017 na akaongoza kuongoza kikosi hicho kutwaa mataji mawili mnamo 2018-19 na 2020-21. Chini ya ukufunzi wake, Ajax walitinga nusu-fainali za UEFA mnamo 2018-19 ambapo walidenguliwa na Spurs.

Zaidi ya Ten Hag, wakufunzi wengine waliokuwa wakihusishwa na mikoba ya Man-United ni kocha wa zamani wa Spurs ambaye sasa ananoa kikosi cha Paris St-Germain (PSG) Mauricio Pochettino na Julen Lopetegui wa Sevilla wanaoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Ten Hag anatarajiwa kuleta katika benchi yake ya kiufundi kocha wa zamani wa Man-United au mchezaji wa zamani wa kikosi hicho kuwa msaidizi wake ikizingatiwa kwamba Mike Phelan ambaye sasa ni msaidizi wa Rangnick ana uhusiano wa karibu na Solskjaer. Rangnick ambaye ni raia wa Ujerumani, anatazamiwa kusalia ugani Old Trafford kushauri benchi ya kiufundi itakayoongozwa na Ten Hag.

Ten Hag alijiunga na Ajax baada ya kuhudumu kambini mwa Utrecht kwa kipindi cha miaka miwili na nusu. Awali, alikuwa amedhibiti mikoba ya kikosi cha pili cha Bayern Munich ambapo alifanya kazi na kocha wa sasa wa Manchester City, Pep Guardiola aliyekuwa mkufunzi mkuu wa kikosi cha kwanza cha Bayern nchini Ujerumani.

Solskjaer alitimuliwa na Man-United mnamo Novemba 2021 baada ya kikosi hicho kupokezwa na Watford kichapo cha 4-1 ugani Vicarage Road. Matokeo hayo yalisaza Man-United katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

Tangu Rangnick apokezwe mikoba ya Man-United mnamo Disemba 3, 2021, kikosi hicho kimeshinda mechi tisa, kuambulia sare mara sita na kupoteza michuano minne kati ya 19 katika EPL.

Aidha, walibanduliwa na Atletico Madrid kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA baada ya Middlesbrough ya Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship) kuwadengua kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA.

Baada ya kichapo cha 4-0 kutoka kwa Liverpool mnamo Aprili 19, 2022 ugani Anfield, Rangnick alisema alihitaji kusalia kikosini na wanasoka 10 pekee kambini mwa Man-United mwishoni mwa msimu huu.

Mnamo Aprili 20, 2022, Man-United walitangaza kuwa maskauti wakuu wa vipaji kambini mwao, Jim Lawlor na Marcel Bout, walikuwa wameagana rasmi na kikosi.

Man-United walijizolea jumla ya mataji 38 chini ya kocha Ferguson aliyedhibiti mikoba yao ya ukufunzi kwa miaka 26 ugani Old Trafford. Kati ya mataji hayo ni 13 ya EPL, mawili ya UEFA, matano ya FA na manne ya League Cup au Carabao Cup.

Hata hivyo, tangu kustaafu kwake mnamo 2013, Man-United wameshinda Kombe la FA mara moja pekee chini ya Louis van Gaal; League Cup, Europa League na Community Shield chini ya Jose Mourinho; na Charity Shield chini ya David Moyes.

Moyes, aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Ferguson kwa muda mrefu, alipokezwa mkataba wa miaka sita kabla ya kupigwa kalamu katika msimu wake wa kwanza ugani Old Trafford.

Ten Hag anatarajiwa kukifanyia kikosi cha Man-United mabadiliko makubwa na kuongoza mchakato wa kusajili wanasoka wapya chini ya mkurugenzi wa masuala ya soka John Murtough, mkurugenzi wa kiufundi Darren Fletcher na afisa mkuu mtendaji Richard Arnold.

WAKUFUNZI WA AWALI WA MAN-UNITED (kwa mikataba ya kudumu) TANGU KUSTAAFU KWA FERGUSON:

Kocha Tarehe Idadi Ya Mechi Asilimia Ya Kushinda

 

1 David Moyes Julai 2013-Aprili 2014 51 53%

 

2 Luois van Gaal Mei 2014-Mei 2016 103 52%

 

3 Jose Mourinho Mei 2016-Disemba 2018 144 58%

 

4 Ole Gunnar Solskjaer Disemba 2018-Novemba 2021 168 54%

 

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Man-City wapepeta Brighton na kurejea kileleni mwa jedwali...

Serikali yatakiwa itume polisi kulinda mali ya Mumias

T L