• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:35 AM
Man-United wamsajili fowadi Wout Weghorst wa Uholanzi kwa mkopo

Man-United wamsajili fowadi Wout Weghorst wa Uholanzi kwa mkopo

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wamemsajili fowadi matata raia wa Uholanzi, Wout Weghorst kwa mkopo kutoka Burnley.

Weghorst alihudumu kambini mwa Besiktas kwa nusu ya msimu huu wa 2022-23 na sasa ametua ugani Old Trafford alikofanyiwa vipimo vya afya baada ya mkataba wake wa mkopo wa msimu mmoja kambini mwa Besiktas ya Ligi Kuu ya Uturuki kutamatishwa.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 30 alifunga mabao manane na kuchangia mengine manne kutokana na mechi 16 alizochezea Besiktas.

Bao lake la hivi karibuni zaidi lilitokana na mechi iliyoshuhudia Besiktas wakipepeta Kasimpasa 2-1 katika Ligi Kuu ya Uturuki mnamo Januari 7, 2023. Alitumia mchuano huo kuwaaga mashabiki na wachezaji wenzake kambini mwa Besiktas.

Kusajiliwa kwa Weghorst kunampa kocha Erik ten Hag chaguo la kumchezesha na Marcus Rashford au Anthony Martial katika safu ya mbele ya Man-United wanaojivunia ufufuo mkubwa wa makali yao.

Weghorst alifunga mabao mawili ya dakika za mwisho katika mechi iliyokutanisha Uholanzi na Argentina katika robo-fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.

Alifunga pia mkwaju wa penalti katika mchuano huo ambao Argentina walishinda katika safari yao ya kutawazwa mabingwa kwa kupepeta Ufaransa 4-2 kwenye fainali mnamo Disemba 18, 2022.

Weghorst alifunga mabao mawili katika mechi 20 alizochezea Burnley waliomsajili kutoka Wolfsburg miezi 12 iliyopita. Hata hivyo, mchango wake huo haukusaidia Burnley kutoteremshwa ngazi kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship).

Weghorst huenda akawajibishwa na Man-United dhidi ya Manchester City katika gozi la EPL litakalowakutanisha ugani Old Trafford mnamo Januari 14, 2023.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto anyonga bajeti ya sekta muhimu kwa Sh90 bilioni

Barcelona kuvaana na Real Madrid kwenye fainali ya Spanish...

T L