• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Mashabiki wa Schalke washambulia kikosi kwa mayai baada ya kuteremshwa ngazi kwenye Bundesliga

Mashabiki wa Schalke washambulia kikosi kwa mayai baada ya kuteremshwa ngazi kwenye Bundesliga

Na MASHIRIKA

WANASOKA wa Schalke pamoja na maafisa wao wa benchi ya kiufundi walishambuliwa na mashabiki wao wenyewe waliowarushia mayai baada ya kikosi hicho kuteremshwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 33.

Schalke walishushwa daraja kwenye kipute cha Bundesliga msimu huu baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa limbukeni Arminia Bielefeld. Mechi hiyo ilikuwa yao ya 21 kupoteza kwenye kampeni za muhula huu.

Mnamo Jumatano, zaidi ya mashabiki 600 waliingia katika uwanja wa Schalke Stadium na kuwavamia wachezaji pamoja na vinara wa kikosi hicho huku wakiwazomea na kuwarushia mayai.

Kabla ya kujitoma ugani, mashabiki hao ambao sehemu kubwa walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi mjini Gelsenkirchen, walikua wamewasha moto mkubwa nje ya uwanja huku wakifyatua fataki.

Schalke walioambulia nafasi ya pili kwenye kampeni za Bundesliga mnamo 2018, ni miongoni mwa vikosi vinavyojivunia idadi kubwa ya mashabiki nchini Ujerumani na kila mojawapo ya mechi zao za nyumbani huvutia zaidi ya mashabiki 60,000 ugani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Keki anazooka zinapendwa na wateja kote nchini

Man-City sasa wanahitaji alama nane pekee kutokana na mechi...