• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Matano roho juu CS Sfaxien ikiwasili, Gor ziarani Congo

Matano roho juu CS Sfaxien ikiwasili, Gor ziarani Congo

Na CECIL ODONGO

Kocha wa Tusker Robert Matano amesema kuwa timu hiyo haiogopi wapinzani wao CS Sfaxien ambao waliwasili nchini jana kuelekea mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Mashirikisho (Caf) mnamo Jumapili.

Wakati huo huo, wawakilishi wengine wa Kenya kwenye mashindano hayo, Gor Mahia wanaondoka nchini leo saa 11 asubuhi hadi Congo Brazzaville kwa mechi yao ya Caf dhidi ya AS Otoho d’Oyo.Kuhusu mechi ya Tusker, jana kikosi cha watu 35 ambacho kinajumuisha wachezaji pamoja na wanachama wa benchi ya kiufundi waliwasili nchini kupitia ndege ya Shirika la Qatar.

Timu huyo chini ya Kocha Mwitaliano Giovanni Solinas ambaye ana umri wa miaka 53, inatarajiwa itatoa upinzani mkali kwa Tusker ambayo imekuwa na rekodi duni dhidi ya timu za Kaskazini mwa Afrika.Hata hivyo, Matano jana alisema kuwa hawaogopi wapinzani wao na lengo lao ni kupata ushindi hapa nyumbani kisha kumalizia kazi ugenini.

Kocha huyo alisema kuwa dhidi ya Zamalek SC ya Misri ambapo walibanduliwa kwa jumla ya 5-0, timu hiyo ilikuwa na wachezaji wapya ambao hawakuwa wameelewana vyema uwanjani.“Hata kama hatujawahi kucheza dhidi yao, nimekuwa nikiwafuatilia na ni kati ya timu bora zaidi nchini Tunisia.

Hata hivyo, sisi hatuwaogopi kwa sababu mpira husakatwa uwanjani na lengo letu ni kushinda,” akaeleza Taifa Leo. Aliongeza kuwa wachezaji wake wote sasa wako sawa wala hawana jeraha ila beki wake Jimmy Mbugua amepona japo bado hayupo fiti kusakata mechi hiyo.

“Wachezaji wako sawa na hatungependa kile kilichotokea dhidi ya Zamalek kitokee tena. Kwa sasa lazima tujitume na kupata ushindi nyumbani kwa sababu hata sisi lengo letu ni kutinga awamu ya makundi,” akaongeza.Kuhusu Gor, Mkurugenzi wa Michezo Lordvick Aduda ambaye tayari yuko Congo, alisema maandalizi yote yamekamilika kuhusu mechi hiyo wachezaji wa Gor wakitua nchini humo leo.

“Tumekodisha hoteli, uwanja pia haupo mbali na ratiba yote iko sawa. Wenyeji wetu pia wametupa basi ambalo litatusaidia katika masuala ya usafiri,” akasema Aduda kutoka Congo.Mechi ya Gor dhidi ya AS Otoho inatarajiwa kuanza saa 11.30 jioni huku ile ya Tusker ambayo itahudhuriwa na mashabiki ikianza saa tisa, zote zikisakatwa mnamo Jumapili.

You can share this post!

Mbunge Hassan aomba baraza la kiswahili kubuniwa nchini

Kocha wa Sugar RFC hofu vifaa tegemeo kukosekana ufunguzi...

T L