• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Matasi aahidi kusaidia Tusker FC kuzoa mataji baada ya kumsaini kwa kandarasi ya miaka miwili

Matasi aahidi kusaidia Tusker FC kuzoa mataji baada ya kumsaini kwa kandarasi ya miaka miwili

Na GEOFFREY ANENE

“KAZI ianze sasa.”

Huo ni ujumbe kutoka kwa kipa Patrick Musotsi Matasi baada ya kuajiriwa tena na mabingwa wa Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) hapo Agosti 28.

Matasi amesaini kandarasi ya miaka miwili na klabu hiyo aliyoichezea kati ya Julai 1 mwaka 2018 hadi Oktoba 18, 2018.

Mwezi Aprili, tetesi zilidai kuwa kipa huyo mwenye umri wa miaka 33 alikaribia kujiunga na miamba wa Tanzania, Simba SC kutoka miamba wa Ethiopia, Saint George. Hiyo ilikuwa wiki chache kabla ahusike katika ajali mbaya na familia yake mapema mwezi Juni. Kandarasi yake na Saint George ilikatika Juni mwisho na amekuwa huru kujiunga na klabu yoyote.

“Tungependa kuthibitisha kuwa kipa Patrick Matasi amejiunga tena na timu hii kwa kandarasi ya miaka miwili. Kipa huyu anarejea Tusker baada ya misimu mitatu akichezea Saint George nchini Ethiopia. Atavalia jezi nambari 34,” Tusker ilitangaza kupitia mtandao wake.

“Nafurahi sana kuwa tena mchezaji wa Tusker na ni heshima kubwa. Nilichezea Tusker miezi mitatu pekee na kuondoka na kurejea kwangu hapa kunamaanisha kuwa kuna kitu nataka kutimiza kama mchezaji. Niko hapa kufanya kazi na kusaidia timu kupata mafanikio na kutimiza malengo yake,” alisema Matasi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Kabras United, Posta Rangers na AFC Leopards aliongeza, “Najiunga na timu nzuri ambayo imepata ufanisi mkubwa. Tusker imeshinda ligi na itawakilisha Kenya katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na hiki ni kitu muhimu sana kwa mchezaji. Lazima nijitahidi kupigania klabu hii.”

Akimkaribisha kipa huyo, mwenyekiti wa Tusker FC Dan Aduda alisema, “Tuna furaha asana kupata huduma za Matasi. Ataongeza ushindani katika idara ya makipa. Amewahi kuwa hapa hapo awali, anajua klabu hii inasimamia nini na haitakuwa vigumu kwake kuzoea mazingira haya mapya.”

Afisa Mkuu Mtendaji Charles Obiny aliongeza, “Tunapojiandaa kushiriki Klabu Bingwa Afrika, ujuzi wa Matasi utakuwa muhimu kwa idara ya makipa. Ameshiriki mashindano makubwa katika kiwango cha klabu na pia na timu ya taifa. Yeye ni sajili muhimu kwa kikosi chetu.”

Matasi amechezea Harambee Stars zaidi ya michuano 20 ikiwemo katika Kombe la Afrika 2019.

Mchuano wake wa kwanza akivalia jezi ya Harambee Stars ulikuwa dhidi ya Uganda mnamo Machi 23 mwaka 2017. Aliibuka kipa bora wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) mnamo Desemba 2017.

You can share this post!

Siogopi vitisho vya serikali

Real Madrid wapiga Betis na kutua kileleni mwa jedwali la...