• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
MBWEMBWE: Licha ya ukwasi wa Sh4.6b Alba aendelea kuchuma zaidi

MBWEMBWE: Licha ya ukwasi wa Sh4.6b Alba aendelea kuchuma zaidi

Na CHRIS ADUNGO

JORDI Alba, 32, ni beki wa kushoto wa Barcelona na timu ya taifa ya Uhispania.

Alianza kusakata soka akivalia jezi za Barcelona ambao baadaye walimwachilia kutokana na ufupi wa kimo chake. Baada ya kuchezea Cornella (2005-07), Alba aliingia katika sajili rasmi ya Valencia waliojivunia maarifa yake kwa kipindi cha miaka sita kabla ya kurejea uwanjani Camp Nou kuwasakatia Barcelona mnamo 2012.

Tangu wakati huo, Alba amewaongoza waajiri wake kutwaa mataji 14 yakiwemo matano ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), manne ya Copa del Rey na moja la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Baada ya kunyanyua mataji 23 na kufunga bao moja akivalia jezi za chipukizi kambini mwa Uhispania, Alba alianza kuwajibikia kikosi cha watu wazima cha Uhispania mnamo 2011 na akwa sehemu ya timu iliyotwaa ufalme wa Euro 2012. Alikuwa pia tegemeo kwenye fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia mnamo 2014 na 2018.

UTAJIRI

Soka iliyopigwa na Alba kambini mwa Valencia kati ya 2007 na 2012 ilichangia pakubwa utajiri wake ambao kwa sasa unamweka katika nafasi ya 71 kwenye orodha ya wanasoka 100 tajiri zaidi ulimwenguni.

Thamani ya mali yake inakadiriwa kufikia Sh4.6 bilioni na kilichochangajia ukwasi wake ni mshahara wa Sh21 milioni aliokuwa akipokezwa kwa wiki na Valencia kabla ya Barcelona kuzinyakua upya huduma zake kwa malipo ya Sh24 milioni kila wiki mnamo 2012. Barcelona kwa sasa wanamdumisha kwa ujira wa Sh28 milioni kila baada ya siku saba.

Malipo hayo yanamweka Alba katika kundi moja na wanasoka Gerard Pique, Ousmane Dembele, Sergi Roberto na Samuel Umtiti. Hili ndilo kundi la pili la wachezaji wanaolipwa mshahara wa juu zaidi uwanjani Camp Nou baada ya Sergio Busquets, Frenkie de Jong na Antoine Griezmann.

Mgongo wa Alba kimshahara unasomwa kwa karibu sana na kipa Marc-Andre ter Stegen, Junior Firpo na Martin Braithwaite.

Zaidi ya mshahara mkubwa anaolipwa na Barcelona, Alba pia hujirinia fedha za ziada kutokana na marupurupu na bonasi za kushinda mechi akivalia jezi za timu ya taifa ya Uhispania.

Kwa pamoja na Ciro Immobile wa Lazio na timu ya taifa ya Italia, Alba pia ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni ya Electronic Arts (EA Sports) ambayo humkabidhi takriban Sh22 milioni kila mwezi. Yeye pia ni balozi wa mauzo wa kampuni ya Adidas inayompokeza kitita cha takriban Sh130 milioni mwishoni mwa kila mwaka.

MAGARI

Kwa mwanasoka wa haiba yake, Alba anamilki magari mengi ya kifahari ambayo ni pamoja na Lamborghini Urus, Audi R8, Bentley Continental GT, Ferrari 458 Spider na Range Rover Evoque. Thamani ya magari haya yote inakisiwa kufikia Sh98 milioni. Alba alimnunulia mchumba wake Romarey Ventura gari aina ya Audi S9 mnamo Mei mwaka huu alipokuwa akiadhimisha miaka 31 ya kuzaliwa kwake. Gari hilo ilimgharimu Alba kima cha Sh24 milioni.

MAJENGO

Alba alijinunulia kasri la Sh600 milioni katika eneo la Catalonia, Uhispania mwanzoni mwa mwaka wa 2018. Anamiliki majengo mengine mawili ya kifahari anayoyatumia kwa shughuli za kibiashara viungani mwa jiji la Catalonia. Moja kati ya majengo hayo lilimgharimu Sh300 milioni mwanzoni mwa 2019. Alba aliwajengea pia wazazi wa mchumba wake kasri la Sh320 milioni katika eneo la El Viso del Alcor, Uhispania mwishoni mwa 2018.

FAMILIA NA MAPENZI

Alba alizaliwa mnamo Machi 21, 1989 katika eneo la Llobregat, Uhispania. Alianza kutoka kimapenzi na kipusa raia wa Uhispania, Romarey mnamo 2015 na kwa sasa wanapanga kula yamini ya ndoa kufikia Mei 2021. Romarey ni msomi wa masuala ya utalii kutoka Chuo Kikuu cha Seville, Uhispania.

You can share this post!

Raila asaka njia mpya ya Canaan

Maelfu bado wang’ang’ana kutoroka huku hofu ikienea