• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:02 AM
Messi afunga mawili dhidi ya Huesca na kufikia rekodi ya Xavi

Messi afunga mawili dhidi ya Huesca na kufikia rekodi ya Xavi

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga mabao mawili na kuchangia jingine katika ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na Barcelona dhidi ya limbukeni Huesca katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumatatu usiku.

Messi alitumia mchuano huo kufikia rekodi ya jagina XavI Hernandez na sasa wao ndio wanasoka wawili kuwahi kuwajibishwa na Barcelona mara nyingi zaidi (michuano 767) katika historia.

Messi aliwafungulia Barcelona ukurasa wa mabao katika dakika ya 13 kabla ya kuchangia la pili lililojazwa wavuni na fowadi wa zamani wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann katika dakika ya 35. Huesca walifungiwa bao lao na Rafa Mir kupitia penalti ya mwisho wa kipindi cha kwanza kabla ya Barcelona kupachikiwa magoli mengine na Oscar Mingueza na Messi katika dakika za 53 na 90 mtawalia.

Ushindi huo ulikweza Barcelona ya kocha Ronald Koeman hadi nafasi ya pili jedwalini kwa alama 59, nne pekee nyuma ya viongozi Atletico Madrid wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone.

Mabingwa watetezi Real Madrid wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 57, sita mbele ya Sevilla wanaofunga orodha ya nne-bora. Huesca kwa upande wao wanavuta mkia baada ya kujizolea alama 20 pekee kutokana na mechi 27 za hadi kufikia sasa msimu huu.

Messi, 33, ameongoza Barcelona kutia kapuni mataji 10 ya La Liga na manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kati ya makombe 34 anaojivunia kunyanyua akivalia jezi za kikosi hicho kilichomwajibisha kwa mara ya kwanza katika ushindi wa 1-0 waliousajili dhidi ya Espanyol mnamo Oktoba 16, 2004.

Messi ambaye mkataba wake wa sasa na Barcelona unatamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu, atavunja rekodi ya Xavi ambaye ni kiungo wa zamani wa Uhispania iwapo kocha Koeman atamchezesha dhidi ya Real Sociedad mnamo Machi 21, 2021.

Barcelona walibanduliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa katika hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Machi 10, 2021. Hata hivyo, wangali na matumaini ya kutawazwa wafalme wa La Liga na Copa del Rey muhula huu. Kikosi hicho tayari kimefuzu kwa fainali ya Copa del Rey ambapo kitavaana na Athletic Bilbao mnamo Aprili 3, 2021.

Huesca waliwahi kupokezwa na Barcelona kichapo cha 8-2 uwanjani Camp Nou katika mechi ya La Liga mnamo 2018. Zimesalia mechi 11 pekee kwa kampeni za La Liga msimu huu kutamatika rasmi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Kadhi Mkuu mpya sasa atoke eneo jingine la...

Diogo Jota afunga kuweka hai matumaini ya Liverpool kucheza...