• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mjamaica matata Shelly-Ann Fraser-Pryce aingia Kip Keino Classic

Mjamaica matata Shelly-Ann Fraser-Pryce aingia Kip Keino Classic

Na GEOFFREY ANENE

WATIMKAJI matata wa mbio fupi Shelly-Ann Fraser-Pryce na Sha’Carri Richardson ni wanariadha wa hivi punde wa kigeni kuthibitisha watashiriki mashindano ya kimataifa ya Kip Keino Classic jijini Nairobi mnamo Mei 7.

Wenyeji wa mashindano hayo yatakayokuwa yakiadhimisha miaka mitatu mwezi ujao, wametangaza kuwa bingwa mara nane wa mataji ya dunia mbio za mita 100 Fraser-Pryce,35, kutoka Jamaica, ambaye pia anajivunia mataifa mawili ya umbali huo ya Olimpiki, na Richardson,22, watamenyana na baadhi ya talanta matata barani Afrika.

Mnamibia Christine Mboma, raia wa Ivory Coast Marie Josee Ta Lou na Mnigeria Aminatou Seyni walitetemesha katika mbio za mita 200 kwenye makala ya pili ya Kip Keino mwaka 2021 ambazo Fraser-Pryce na Richardson watakuwa pia wanashiriki.

Bingwa wa Olimpiki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Peruth Chemutai kutoka Uganda atakuwa akishiriki makala ya tatu mfululizo.

Baadhi ya Wakenya waliotoa ithibati ya kushiriki ni mshindi wa nishani ya shaba mbio za ukumbini za mita 1,500 Abel Kipsang, mshindi wa medali ya dunia mbio za mita 5,000 Margaret Chelimo na malkia mara mbili wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwa watimkaji wasiozidi umri wa miaka 20 Celliphine Chespol.

You can share this post!

Klopp aingia nusu fainali UEFA

Sijajiondoa, nitawania tiketi ya UDA ugavana Kiambu –...

T L