• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Sijajiondoa, nitawania tiketi ya UDA ugavana Kiambu – ‘Jungle’ Wainaina

Sijajiondoa, nitawania tiketi ya UDA ugavana Kiambu – ‘Jungle’ Wainaina

Na LAWRENCE ONGARO

MBUNGE wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amesema bado yupo kwenye kinyang’anyiro cha mchujo kwa tiketi ya ugavana wa Kiambu UDA leo.

Kwa muda wa siku kadha kumekuwepo na uvumi kuwa wameafikiana na seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi ili ajiondoe.

“Ukweli wa mambo ni kwamba hakuna ukweli katika mambo hayo na Mimi naelewa ya kwamba nitajitupa ulingoni kumenyana na wapinzani wangu wawili wakuu,” alifafanua Bw Wainaina.

Wapinzani wake wakuu katika mchujo huo ni seneta wa Kiambu Bw Kimani Wamatangi, na aliyekuwa gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu ambao wote wanaamini pia wana ufuasi mkubwa.

Kwa muda wa wiki moja hivi kumekuwa na uvumi kuwa Bw Wainaina atalazimika kumpisha Bw Wamatangi katika muundo wa maelewano.

Hata hivyo mbunge huyo amesema demokrasia ni lazima ipewe nafasi ili wananchi wafanye uamuzi wao bila kuchaguliwa kiongozi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa kuzuru eneo la Gatundu Kaunti ya Kiambu, kutafuta kura kwa wananchi aliwashauri wapinzani wake waache kuhaha kwani wanaume ni sharti waonane kiwanjani ili kujua mbivu na mbichi.

“Mimi nina imani mchujo huo utakuwa wa wazi na haki pamoja na uwajibikaji. Kwa hivyo kila kiongozi ajitupe mashinani kutafuta kura badala ya kueneza propaganda zisizo na msingi,” alifafanua Bw Wainaina.

Mbunge huyo ameonekana kuwa tisho kubwa kwa wapinzani wake na Kwa hivyo uvumi za aina hiyo ni sharti yapatikane.

Wananchi wamehimizwa kufika na vitambulisho vyao kwani chama cha UDA kitatumia orodha ya tume ya uchaguzi na mipaka ya IEBC ili kugagua wapiga kura.

“Sisi kama viongozi tungeomba uwazi ufuatwe ili uchaguzi uwe wa haki na amani. Mimi kama mbunge wa Thika nikishindwa kwa njia ya haki nitakubali matokeo na nikishinda pia ningetaka itangazwe kwa uwazi,” alijitetea Bw Wainaina wakati wa mahojiano.

  • Tags

You can share this post!

Mjamaica matata Shelly-Ann Fraser-Pryce aingia Kip Keino...

Mwaniaji awataka maajenti wa UDA wawe macho mchujoni

T L