• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Mkufunzi wa kimataifa Shinji Akita awahimiza makocha wa karate wafundishe kwa kujitolea

Mkufunzi wa kimataifa Shinji Akita awahimiza makocha wa karate wafundishe kwa kujitolea

NA LAWRENCE ONGARO

MKUFUNZI wa karate wa kimataifa Shinji Akita, amewahimiza makocha wa hapa nchini wawe makini kusambaza ujuzi waliopata kutoka kwake hivi majuzi.

Mkufunzi huyo alirejea katika makazi yake nchini Ujerumani mnamo Jumanne, huku akipongeza Wakenya kwa kuonyesha ukarimu alipokuwa nchini.

Alisema baada ya kuwa hapa nchini kwa muda mchache amepata ya kwamba kuna vipaji vingi ambapo vikijengwa vyema vinaweza kunawiri.

Mkufunzi huyo ambaye ni mwakilishi mkuu wa shirikisho la mchezo huo Skai- International, alizuru Kenya kwa wiki mbili na kutoa mafunzo mapya kuhusu mchezo wa karate.

Mkufunzi huyo ambaye ni raia wa Japan anayeishi Ujerumani amezuru nchi nyingi ili kutoa mafunzo ya karate.

Baadhi ya nchi alizuru mnamo mwezi Machi na Aprili ni Ufaransa, Kenya, na Uingereza kwa mialiko ya kuendeleza mchezo wa karate.

Wakati wa zoezi nchini Kenya, mkufunzi huyo alishirikiana na mwenzake Martin Klaus ambaye ni raia wa Ujerumani lakini makazi yake ni Mombasa, Kenya.

Aliwahimiza wakufunzi wa Kenya kutumia ujuzi waliopata kukuza wanakarate chipukizi.

Wanakarate wapatao 50 walinufaika pakubwa kwa kupokea mafunzo mapya kuhusu mchezo wa karate.

Shinji Akita (kulia). PICHA | LAWRENCE ONGARO

Wakati wa mazoezi hayo alisisitiza umuhimu wa kujiamini wakati unaposhiriki kwenye mashindano yoyote Ile.

Aliwahimiza pia wanakarate hao kuzingatia nidhamu na kujiamini michezoni.

Wanakarate hao walishauriwa kuzingatia ujuzi na kuwa makini wanapowakabili wapinzani wao.

Aliwahimiza makocha wa karate wahakikishe mchezo huo unakuzwa kutoka vijana wadogo ili wawe na ujuzi kamili.

Baadhi ya wakufunzi walipandishwa gredi ya viwango vya ukanda mweusi kutoka 1st Dan hadi kile cha 4th Dan.

Kabla ya kupokea gredi hiyo wanakarate hao walionyesha ujuzi wao kwa kufuata maagizo waliyopewa na mkufunzi huyo.

  • Tags

You can share this post!

Wahanga sita wa mkasa wa moto Kandara wazikwa katika kaburi...

Ruto, Raila watumia jina la Kibaki kujiuza

T L