• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Mourinho aajiriwa na AS Roma ya Italia wiki mbili baada ya kutimuliwa na Tottenham

Mourinho aajiriwa na AS Roma ya Italia wiki mbili baada ya kutimuliwa na Tottenham

Na MASHIRIKA

JOSE Mourinho ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa kikosi cha AS Roma nchini Italia kuanzia msimu ujao wa 2021-22 na atahudumu kambini mwa klabu hiyo kwa kipindi cha misimu mitatu.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 58 atajaza pengo la Mreno mwenzake, Paulo Fonseca, ambaye Roma wamefichua kwamba ataagana nao rasmi mwishoni mwa kampeni za muhula huu wa 2020-21.

Mourinho anapata kazi kambini mwa Roma ambao ni mabingwa mara tatu wa Serie A, wiki mbili pekee baada ya Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kumtimua mnamo Aprili 19, 2021 kwa sababu ya matokeo duni.

“Uzalendo wa mashabiki wa Roma ni miongoni mwa sababu zilizonichochea kukubali haraka ofa ya kudhibiti mikoba ya kikosi hicho. Nasubiri kwa hamu kuanza kazi na kuanza kushindia klabu hiyo mataji zaidi,” akatanguliza Mourinho.

“Asanteni sana familia ya Friedkin kwa kuniteua kati ya wakufunzi wengi katika ulingo wa soka kwa sasa kuongoza kikosi hiki cha Roma kinachojivunia historia kubwa. Nimekutana na wamiliki na mkurugenzi wa kikosi, Tiago Pinto, ambaye amenifafanulia falsafa na malengo yao,” akaongeza.

Mourinho amewahi pia kudhibiti mikoba ya Inter Milan, Chelsea, Manchester United na Real Madrid nje ya taifa la Ureno.

Mourinho alifutwa kazi na Spurs mnamo Aprili 19, 2021 baada ya kuhudumu kambini mwa klabu hiyo kutoka London Kaskazini kwa kipindi cha miezi 17.

Mechi 10 ambazo alizopoteza ligini msimu huu kambini mwa Spurs ndiyo idadi kubwa zaidi ya michuano kwa Mourinho kushindwa katika historia yake ya ukufunzi.

Alijivunia kipindi cha kuridhisha mara ya mwisho aliponogesha soka ya Serie A kwa kuongoza Inter Milan kutia kapuni jumla ya mataji manne chini ya muda wa misimu miwili.

Mourinho alisaidia kikosi hicho kutwaa mataji mawili ya Serie A, Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Coppa Italia. Ukubwa wa mchango wake kambini mwa Inter ulishuhudia klabu hiyo ikijizolea jumla ya mataji matatu mnamo 2009-10.

Hiyo ilikuwa mara ya mwisho kwa Inter Milan kutwaa ufalme wa Serie A kabla ya kocha Antonio Conte kuwaongoza kukomesha ukiritimba wa Juventus na kujinyanyulia taji la kipute hicho msimu huu wa 2020-21.

Kwa upande wao, Roma hawajawahi kutia kibindoni taji la Serie A tangu 2000-01 walipokuwa chini ya mkufunzi wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Fabio Capello.

Roma walipoteza fainali ya European Cup mnamo 1984 baada ya kuzidiwa maarifa na Liverpool ya Uingereza katika uwanja wao wa nyumbani. Walitawazwa mabingwa wa soka ya bara Ulaya mnamo 1941-42 na 1982-83.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mwilu ahimiza maadili miongoni mwa wanahabari

Rangers yasajili fowadi matata raia wa Zambia, Fashion...