• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mourinho aonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi kati ya AS Roma na Real Betis

Mourinho aonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi kati ya AS Roma na Real Betis

Na MASHIRIKA

KOCHA Jose Mourinho alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi ya kirafiki iliyoshuhudia kikosi chake cha AS Roma kikisalia na wanasoka wanane pekee uwanjani dhidi ya Real Betis ya Uhispania.

Betis walikuwa kifua mbele kwa mabao 3-2 kufikia dakika ya 57 wakati ambapo wachezaji wa Roma waliokuwa ugenini walilalamikia kuwa Alex Moreno alikuwa amenawa mpira ndani ya kijisanduku.

Kiungo Lorenzo Pellegrini wa Roma alionyeshwa kadi nyekundu kwa ubishi mkali naye Mourinho akafurushwa kwa kadi nyekundu baada ya kumchemkia refa kwa kupuuza malalamishi ya wachezaji wake waliokuwa wakidai penalti.

Gianluca Mancini na Rick Karsdorp walionyeshwa kadi za manjano kwa mara nyingine mwishoni mwa mechi na kuwapa Betis fursa ya kuteremkia Roma na kufanya mambo kuwa 5-2 katika mechi hiyo iliyochezewa mjini Seville.

Roma walikuwa awali wametoka nyuma mara mbili kupitia kwa sajili mpya kutoka Uzbek, Eldor Shomurodov aliyefuta juhudi za Rodri kabla ya Mancini kufanya mambo kuwa 2-2 dakika 50 baada ya Nabil Fekir kufunga.

Kizaazaa kilizuka uwanjani baada ya Betis kufungiwa mabao na Moreno, Cristian Tello na Rober na kuzima matumaini ya Roma kurejea mchezoni.

Betis wameratibiwa kuanza kampeni za msimu mpya wa 2021-22 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) dhidi ya Mallorca mnamo Agosti 14, 2021.

Siku hiyo, Roma watanogesha mchuano mwingine wa kirafiki dhidi ya kikosi cha Raja Casablanca kutoka Morocco kabla ya kuanza mchujo wa Europa Conference mnamo Agosti 19 kisha kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) dhidi ya Fiorentina mnamo Agosti 22, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Makundi 10 ya wafanyabiashara Thika yapokea mkopo wa Sh1.4...

Kipa Alisson Becker kuendelea kudakia Liverpool hadi 2027