• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Kipa Alisson Becker kuendelea kudakia Liverpool hadi 2027

Kipa Alisson Becker kuendelea kudakia Liverpool hadi 2027

Na MASHIRIKA

KIPA Alisson Becker amerefusha muda wa kuhudumu kwake ugani Anfield kwa kutia saini mkataba mpya wa hadi 2027.

Mlinda-lango huyo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 28 ni mwingi wa “imani” na “matumaini” kwamba Liverpool itazidi kumkuza kitaaluma tangu ajiunge na kikosi hicho mnamo 2018 baada ya kuagana na AS Roma ya Italia.

Alisson amesaidia Liverpool kutia kapuni taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na jingine lililomchochea kutia saini kandarasi mpya ni kwamba familia yake inafurahia maisha ya mji wa Merseyside.

“Maamuzi ya kusalia Liverpool kwa muda mrefu hayakuwa magumu kufanya. Mambo mengi mazuri hapa Merseyside yalichangia suala hiyo,” akasema Alisson katika mahojiano yake na Liverpoolfc.com.

Alisson ndiye sogora wa hivi karibuni zaidi kutia saini mkataba mpya kambini mwa Liverpool baada ya Fabinho Henrique, 27, anayetarajiwa sasa kuhudumu ugani Anfield hadi 2026.

Mwingine ni beki raia wa Uingereza, Trent Alexander-Arnold, 22, ambaye atachezea Liverpool hadi 2025.

Alisson amewajibishwa na Liverpool mara 130 kufikia sasa na hajafungwa bao katika jumla ya mechi 57 tangu abanduke Roma kwa Sh10 bilioni na kuwa kipa ghali zaidi duniani.

Bao alilofunga mwishoni mwa muda kipindi cha pili dhidi ya West Bromwich Albion mnamo Mei 2021 liliibuka Bao la Msimu la Liverpool mnamo 2020-21. Goli hilo lilimfanya Alisson kuwa kipa wa sita kuwahi kufunga bao katika gozi la EPL na mlinda-lango wa kwanza kuwahi kufanya hivyo kupitia kichwa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mourinho aonyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi kati ya AS...

Spurs wataka Lautaro Martinez wa Inter Milan ajaze pengo la...