• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Mpango wangu ni kurejea Real Madrid na kufikisha usogora wangu katika kiwango cha juu zaidi – Gareth Bale

Mpango wangu ni kurejea Real Madrid na kufikisha usogora wangu katika kiwango cha juu zaidi – Gareth Bale

Na MASHIRIKA

GARETH Bale amesema kwamba mipango yake kitaaluma ni kurejea kambini mwa Real Madrid kuendeleza usogora wake katika kiwango cha juu zaidi mwishoni mwa kipindi chake cha mkopo katika klabu ya Tottenham Hotspur msimu huu.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Wales alirejea Tottenham japo kwa mkopo wa msimu mmoja mwanzoni mwa muhula huu (Septemba 2020).

Fowadi huyo mwenye umri wa miaka 31 angali na mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wake wa sasa na Real ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Anatarajiwa leo kuwa tegemeo kubwa la Wales katika mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 dhidi ya Ubelgiji.

“Hakuna chochote kwa sasa kinachonipotezea dira kitaaluma. Mustakali wangu kitaaluma uko bayana na hauwezi kuathiri matokeo yangu katika timu ya taifa,” akatanguliza.

“Kubwa zaidi katika mipango yangu ni kurejea Real mwishoni mwa msimu huu. Nilirejea Tottenham kwa sababu moja tu – kusakata soka – jambo ambalo ninalifanya kwa sasa,” akaeleza Bale.

“Mpango mwingine ni kutambisha Wales katika kampeni zijazo za Euro na kuongoza timu yangu hii kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia,” akaongeza.

Tangu aingie katika sajili rasmi ya Real, Bale amewaongoza miamba hao kutwaa mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), mawili ya La Liga, moja la Copa del Rey, matatu ya Uefa Super Cup na matatu ya Kombe la Dunia.

Hata hivyo, makali yake yalionekana kushuka katika misimu miwili iliyopita kambini mwa Real baada ya uhusiano wake na kocha Zinedine Zidane kuanza kudorora naye akawa mwepesi wa kupata majeraha mabaya ya mara kwa mara.

Hali hiyo ilichangia marejeo yake kambini mwa Tottenham, kikosi alichojiunga nacho mnamo 2007 baada ya kuagana rasmi na Southampton akiwa na umri wa miaka 17.

Tangu Septemba 2020, amechezea Tottenham mara 25 katika mapambano yote ya msimu huu wa 2020-21 na akapachika wavuni magoli 10.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: ‘Kuwa’ na ‘kua’ yana ukuruba tu wa...

Matokeo mseto kwa mabondia wa Kenya jijini Kinshasa,...