• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:01 AM
Matokeo mseto kwa mabondia wa Kenya jijini Kinshasa, Commander azidi kutisha

Matokeo mseto kwa mabondia wa Kenya jijini Kinshasa, Commander azidi kutisha

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Nick Okoth, Joshua Wasike na George Cosby Ouma walivuna ushindi muhimu kwenye mashindano ya masumbwi ya Afrika ya ukanda wa tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Jumanne.

David Karanja na Martin Aluoch pia walipata ushindi kwenye mashindano hayo yanayotumia mfumo wa mzunguko, lakini bila jasho baada ya kupewa ushindi wa bwerere.

Nao Elly Ajowi na Shaffi Bakari hawakuwa na bahati baada ya kukubali kichapo kutoka kwa Maxime (DR Congo) na Nimuboma Moussa (Burundi).

Okoth maarufu kama Commander, alimlima Kitangila Wa Kitangika (DR Congo) huu ukiwa ni ushindi wake wa pili mfululizo katika uzani wa kilo 57 baada ya kuzidia Aluoch katika siku ya kwanza mnamo Jumatatu.

Wasike alimnyamazisha Ibrahim (Libya) katika uzani wa kilo 91 naye Cosby akabwaga Bolanga Kosa (DR Congo) katika uzani wa kilo 75.

Mambo hayakuwa mazuri kwa kinadada wa Kenya ambapo Christine Ongare pekee ndiye alishinda pigano lake. Ongare, ambaye alikuwa Mkenya wa kwanza kuingia ulingoni Jumanne, alimlemea Havyarimana Ornella (Burundi) katika pigano lake la kwanza kwenye uzani wa kilo 52.

Lucy Stacy Achieng’ hakuwa na lake dhidi ya Tshamala Muenge (DR Congo) katika uzani wa kilo 60, Elizabeth Akinyi alipanguliwa na Acindan Panguana (Msumbiji) katika uzani wa kilo 69 naye Elizabeth Andiego akachapwa na Mwika Marie Joel (DR Congo) katika uzani wa kilo 75.

Mashindano haya ya mataifa saba yanaingia siku ya tatu Jumatano.

Ratiba ya Machi 24:

Kilo 75 – Rudy Gramane (Msumbiji) vs Elizabeth Andiego

Kilo 69 – Helene Makwikila (DR Congo) vs Elizabeth Akinyi

Kilo 60 – Stacy Achieng’ vs. Yumba Therese

Kilo 51 – Christine Ongare vs Munga Zalia (DR Congo)

Kilo zaidi ya 91 – Elly Ajowi vs Saad Saad (Libya), Joshua Wasike vs Jeannot Mutombo

Kilo 81 – Hezron Maganga (Kenya) vs Pogba Nkulu (DR Congo)

Kilo 75 – George Cosby (Kenya) vs El Magabsi (Libya), Styven Mouandza (DR Congo) vs Edwin Okongo (Kenya)

Kilo 63 – Joseph Shighali (Kenya) vs Alain Christian Sangue (Cameroon)

Kilo 52 – Okashash (Libya) vs Shaffi Bakari (Kenya), Nimuboma Moussa (Burundi) vs David Karanja (Kenya)

You can share this post!

Mpango wangu ni kurejea Real Madrid na kufikisha usogora...

AFCON: Atawika nani kati ya Olunga na Mo’ Salah?