• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:50 AM
Mshambuliaji Memphis Depay sasa ni mali ya Barcelona

Mshambuliaji Memphis Depay sasa ni mali ya Barcelona

Na MASHIRIKA

FOWADI matata wa timu ya taifa ya Uholanzi, Memphis Depay, ameafikiana na vinara wa Barcelona kwamba atajiunga rasmi na miamba hao wa soka ya Uhispania baada ya mkataba wake wa sasa na Olympique Lyon ya Ufaransa kutamatika mwisho wa mwezi huu wa Juni.

Barcelona pia wametangaza kwamba Depay, 27, ataingia katika sajili yao kwa mkataba wa miaka miwili utakaotiwa saini baada ya kukamilika kwa fainali za Euro ambazo sogora huyo anashiriki kwa sasa akivalia jezi za Uholanzi.

Depay alifunga bao mnamo Juni 17 na kuongoza Uholanzi kutinga hatua ya 16-bora kwenye Euro baada ya kikosi hicho kuvuna ushindi wa 2-0 dhidi ya Austria.

Katika kipindi cha misimu minne ambapo amehudumu kambini mwa Lyon, Depay amefunga jumla ya mabao 76 kutokana na mechi 178.

Alihamia Ufaransa kunogesha Ligi Kuu ya taifa hilo (Ligue 1) mnamo 2017 baada ya nyota yake kukosa kung’aa kambini mwa Manchester United waliomsajili kutoka PSV Eindhoven ya Uholanzi.

Uhamisho wa Depay hadi Barcelona ulitarajiwa kufaulu hasa ikizingatiwa kwamba sogora huyo aliwahi kukiri kuwa matamanio yake ya muda mrefu kitaaluma yamekuwa ni kunolewa na kocha Ronald Koeman kambini mwa Barcelona.

Koeman aliwahi kumpokeza Depay malezi ya soka wakati akidhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Uholanzi.

Depay anakuwa mchezaji wa nne kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona muhula huu baada ya kikosi hicho kinachojisuka upya chini ya mwenyekiti Joan Laporta kujinasia huduma za wanasoka Sergio Aguero na Eric Garcia kutoka Barcelona.

Barcelona pia wamesajili upya beki raia wa Brazil, Emerson Royal mwenye umri wa miaka 22 kutoka Real Betis ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Emerson aliwahi kuchezea Barcelona baada ya kuagana na kikosi cha Atletico Mineiro cha Brazil mnamo Januari 2019.

Hata hivyo, alitumwa kwa mkopo hadi kambini mwa Betis ambayo ilimpokeza mkataba wa kudumu mwishowe.

Emerson amewajibikia Betis katika mapambano yote na kufungia kikosi hicho jumla ya mabao matano na kuchangia mengine 10.

Ndiye mwanasoka aliyesakata idadi kubwa zaidi ya michuano katika msimu wa 2020-21 chini ya kocha Manuel Pellegrini aliyewaongoza Betis kuambulia nafasi ya sita kwenye La Liga na hivyo kufuzu kwa soka ya Europa League.

Emerson amewakilisha Brazil katika mapambano kadhaa ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 na miaka 23 kabla ya kuwajibishwa kwa mara ya kwanza katika timu ya watu wazima mnamo Novemba 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Roho mkononi wanavoliboli wa Kenya wakipimwa corona Morocco

Homeboyz yalimwa winga wake David Odhiambo akitawazwa...