• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
‘Muuaji’ De Bruyne aweka Man City pazuri

‘Muuaji’ De Bruyne aweka Man City pazuri

NA MASHIRIKA

WOLVEHAMPTON, Uingereza

KEVIN De Bryune aliongoza Manchester City kupiga hatua kubwa katika juhudi zao za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), baada ya kufunga mabao manne wakinyonga Wolves 5-1 mnamo Jumatano.

Katika mchuano huo wa raundi ya 36 ugani Molineux, City iliandikisha historia kwa kuwa timu ya kwanza kuzoa ushindi wa angaa mabao matatu mara tano mfululizo.

Vijana wa kocha Pep Guardiola walifungua ukurasa wa mabao dakika ya saba De Bryune alipoanzisha mashambulizi kwa kumegea Bernardo Silva mpira kabla ya kurudishiwa na kukamilisha kwa ustadi dakika ya saba.

Sherehe za City zilikatizwa dakika nne baadaye “mbwamwitu” wa Wolves waliposawazisha pale gongagonga za Raul Jimenez na Pedro Neto zilikamilishwa na Leandro Dendoncker.

De Bryune aliweka City kifua mbele 2-1 dakika ya 16 baada ya kipa Jose Sa kuondosha mpira wa kiungo huyo kwa Raheem Sterling, uliomrudia Mbelgiji huyo akahakikisha fursa hiyo haipotei.

Alipachika goli lake la tatu dakika ya 24 kutokana na pasi ya Sterling kabla ya kuongeza la nne dakika ya 60. Sterling alihitimisha mvua hiyo ya mabao dakika ya 84 akiweka la tano la City.

“Nafurahi sana; tungepata magoli hata zaidi. Ulikuwa mchezo mzuri kabisa kutoka kwa wachezaji wote,” alitanguliza kocha Guardiola.

“Tunahitaji alama nne zaidi ili kuwa mabingwa, na tutajaribu kupata tatu Jumapili (dhidi ya West Ham). Bado tuna kibarua dhidi ya West Ham na Aston Villa,” akaongeza.

De Bruyne alikiri kwamba bado wana machungu ya kubanduliwa na Real Madrid katika nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), lakini lazima maisha yaendelee.

Alisema: “Sasa lililobaki ni kujizatiti kushinda ligi.”

Katika michuano mingine Jumatano usiku, Chelsea ililemea watu 10 Leeds 3-0 kupitia mabao ya Mason Mount, Christian Pulisic na Romelu Lukaku.

Daniel James alionyeshwa kadi nyekundu upande wa Leeds, inayoning’inia katika mduara wa kutemwa EPL mwisho wa msimu.

Watford na Everton zilitoka 0-0 nayo Leicester ikararua Norwich 3-0 kupitia mabao ya Jamie Vardy (mawili) na James Maddison.

City inaongoza jedwali la EPL kwa alama 89.

Liverpool ina 86 nayo Chelsea 70. Nambari nne Arsenal na tano Tottenham walimenyana jana Alhamisi usiku ambapo Spurs ilipata ushindi wa 3-0.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Ufafanuzi zaidi kuhusu Gredi ya 7 wahitajika

TUSIJE TUKASAHAU: Ruto awe na msimamo thabiti kuhusu SGR

T L