• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Muungano wa wanasoka wa Uruguay wataka FA ibatilishe adhabu ya Cavani

Muungano wa wanasoka wa Uruguay wataka FA ibatilishe adhabu ya Cavani

Na MASHIRIKA

MUUNGANO wa wachezaji wa timu ya taifa ya Uruguay (AFU) wamelitaka Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kubatilisha adhabu ambayo nyota Edinson Cavani alipewa.

Mfumaji huyo wa Manchester United alipigwa marufuku ya mechi tatu na kutozwa faini ya Sh14 milioni kwa ujumbe wa kiuchochezi na wa matusi aliouandika kwa Kihispania na kupakia kwenye akaunti yake ya mtandao wake wa kijamii wa Instagram.

Kati ya wachezaji ambao wamekuwa mstari wa mbele kushinikiza FA kubatilisha adhabu hiyo ya Cavani kwa madai kwamba ni ya kiubaguzi ni Luis Suarez wa Atletico Madrid (Uhispania) na Diego Godin wa Cagliari nchini Italia.

Shirikisho la Soka la Uruguay (AUF) pia limetaka adhabu hiyo ya FA kutathminiwa upya.

Godin ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Uruguay na Suarez wamesambaza barua za AUF na AFU kupitia akaunti zao za mtandao wa Twitter kwa nia ya kushinikiza FA kulegeza adhabu ya Cavani huku wakisisitiza kwamba ukali wa adhabu aliyopokezwa hauwiani na ukubwa wa kosa lake.

Kwa mujibu wa mojawapo ya barua iliyotiwa saini na muungano wa timu wa hiyo ya taifa kutoka Amerika ya Kusini, “hatua ya FA dhidi ya Cavani inakinzana na desturi na tamaduni za Uruguay.”

“Cavani hajawahi kuonyesha mienendo wala kutenda jambo lolote ambalo linaweza kufasiriwa kuwa la kiuchochezi au la kuendeleza ubaguzi wa rangi,” ikasema sehemu ya taarifa ya AFU.

Hata hivyo, FA imesisitiza kwamba “adhabu ya Cavani ilitolewa kwa misingi ya haki baada ya uchunguzi uliohusisha pia mtaalamu wa lugha ishara kuhusishwa katika kufasiri ujumbe uliopakiwa na sogora huyo wa zamani wa PSG mtandaoni.”

Man-United ambao ni waajiri wa Cavani kwa sasa wamesema kwamba mshambuliaji huyo amekubali adhabu aliyopokezwa na FA na aliteua kutokata rufaa “kwa heshima ya kanuni zinazodhibiti mienendo ya wachezaji wanaotandaza soka ya Uingereza na hofu ya kutoonekana kupinga juhudi za FA katika kukabiliana na visa vya ubaguzi wa rangi.”

FA ilimshtaki Cavani mnamo Disemba 17 kwa hatia ya kutumia maneno ambayo katika baadhi ya miktadha, yangefasiriwa kuwa na ujumbe kuwakosea walengwa heshima.

Cavani alipakia ujumbe huo mtandaoni baada ya kufunga bao la ushindi wa 3-2 dhidi ya Southampton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Novemba 29, 2020. Nyota huyo wa zamani wa Napoli alifuta ujumbe huo pindi baada ya ‘uchochezi’ na ‘matusi’ katika baadhi ya maneno aliyotumia kubainika.

Zaidi ya marufuku na faini, Cavani atatakiwa pia kukamilisha kozi ya ana kwa ana ya mafunzo kuhusu nidhamu.

Kutokana na marufuku aliyopiga, Cavani alikosa mechi ya EPL iliyokutanisha Man-United na Aston Villa mnamo Januari 1 na atakosa pia nusu-fainali ya Carabao Cup itakayowakutanisha waajiri wake na Manchester City mnamo Januari 6 na mchuano wa raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Watford mnamo Januari 9.

You can share this post!

Southampton yaipokeza Liverpool kichapo cha 1-0

Mbunge ataka wakazi Buxton wahusishwe kikamilifu katika...