• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Ni mapema sana kwa Manchester United kuanza kuwazia kutwaa taji la EPL msimu huu – Rashford

Ni mapema sana kwa Manchester United kuanza kuwazia kutwaa taji la EPL msimu huu – Rashford

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Marcus Rashford amesema “haitakuwa busara” kwa Manchester United kuanza kufikiria kuhusu uwezekano wa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2020-21.

Hii ni licha ya ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Aston Villa mnamo Ijumaa kupaisha ‘The Red Devils’ hadi kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama sawa na mabingwa watetezi Liverpool ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Southampton mnamo Januari 4, 2021 ugani St Mary’s.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United kwa sasa wanajivunia alama 33, japo ni alama saba pekee ndizo zinawatenganisha na Manchester City na Chelsea ambao ni miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la EPL msimu huu.

Nafasi ya inayoshikiliwa sasa na Man-United jedwalini ndiyo bora zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kukamata kufikia hatua kama hii kwenye kampeni za EPL tangu aliyekuwa kocha wao Sir Alex Ferguson astaafu mnamo 2013.

“Hatuwezi kuanza kuwazia ufalme sasa hivi. Kikosi cha Man-United bado kinahitaji kazi nyingi ya kufanywa na kosa kubwa litakuwa ni kupotezewa dira na nafasi nzuri tunayoishikilia kwa sasa jedwalini,” akatanguliza Rashford.

“Itatulazimu kumakinikia mechi baada ya nyingine na iwapo tutaendeleza ubabe tunaojivunia kwa sasa na kushinda takriban kila mchuano, basi tutajitathmini upya na kuanza kujiwekea malengo ya kunyanyua taji la EPL kuelekea mwisho wa msimu,” akaongeza mfumaji huyo raia wa Uingereza.

Kwa upande wake, Solskjaer amesema hawezi kuzungumzia kuhusu uwezekano wa kikosi chake kutwaa taji la msimu huu hadi kampeni itakapofikia mechi 30.

“Ni vigumu sana kubashiri mshindi wa taji la EPL msimu huu baada ya mechi 16 pekee. Ushindani ni mkali na alama zinazotenganisha vikosi 10 vya kwanza jedwalini ni chache mno,” akasema kocha huyo raia wa Norway.

“Hali ilivyo, huenda mshindi wa muhula huu akaanza kubainika hata baada ya kupigwa kwa michuano 30. Vikosi vingi vimeanika azma ya kutwaa ubingwa na huenda wapinzani wakabadilishana uongozi wa jedwali mara nyingi kabla ya mfalme kuanza kubainika,” akaongeza Solskjaer.

Tangu wapigwe 1-0 na Arsenal uwanjani Old Trafford mwanzoni mwa Novemba 2020, Man-United wameshinda michuano minane kati ya 10 iliyopita ligini.

You can share this post!

WASONGA: Serikali igharimie kuunda maski za kuwatosha...

MUTUA: Weka mipango ya maisha sio tu maazimio ya mwaka