• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 11:48 AM
NI OGIER! Mfaransa Ogier atwaa ubingwa wa WRC Safari Rally

NI OGIER! Mfaransa Ogier atwaa ubingwa wa WRC Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

MFARANSA Sebastien Ogier amefungua mwanya wa alama 34 juu ya jedwali la Mbio za Magari Duniani (WRC).

Hii ni baada ya kuongoza timu ya Toyota kufagia nafasi mbili za kwanza akishinda duru ya Safari Rally siku ya mwisho iliyohudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta na Mawaziri Amina Mohamed (Michezo) na Najib Balala (Utalii), miongoni mwa viongozi wengine, katika eneo la Naivasha, jana.

Mkenya Onkar Rai aliibuka mshindi wa Safari Rally wa kitengo cha daraja ya tatu (WRC3) akiendesha gari la Volkswagen Polo alipokamilisha katika nafasi ya saba mnamo Jumapili.

Bingwa mara saba duniani Ogier akishirikiana na Mfaransa mwenzake Julien Ingrassia, hawakutarajiwa kabisa kutawala Safari Rally. Hii ni baada ya gari lao la Toyota Yaris kuharikibika “suspension” mnamo Juni 25 wakati madereva wengi walitaabika katika mkondo wa Kedong.

Hata hivyo, Ogier, ambaye alikuwa amenyakua mkondo wa kufungua mashindano wa Kasarani wa kilomita 4.84 jijini Nairobi hapo Juni 24, aliendelea kuimarika baada ya kurekebisha gari lake.

Alinyakua mkondo wa Oserian 2 (kilomita 18.87), Soysambu 1 (20.33km), Sleeping Warrior1 (31.04km) na Elementaita2 (14.67km) na kuingia siku ya mwisho ya mashindano hayo ya kilomita 320.19 akiwa nyuma ya kiongozi Thierry Neuville (Hyundai) na Takamoto Katsuta (Toyota).

Ogier alinufaika kurukia nafasi ya pili wakati kiongozi Thierry Neuville alijiuzulu gari lake la Hyundai i20 lilipovunjika “suspension” katika mkondo wa 14 baada ya kukwaruza jiwe m apema jana.

Neuville alikuwa ameanza Jumapili karibu dakika moja mbele ya Katsuta (Toyota Yaris). Ogier aliishia kushinda mkondo huo wa Loldia1 (11.33km).

Elfyn Evans (Toyota Yaris) na Adrien Fourmaux (Ford Fiesta) walitawala mikondo ya 15 (Hell’s Gate1) na 16 (Malewa), mtawalia.

Baada ya mikondo hiyo 16 ya kwanza, Ogier na Mjapani Katsuta walikuwa bega kwa bega uongozini kwa saa 3:04:21.4 dhidi ya Tanak (3:05:30.8) na Fourmaux (3:05:58.5). Ogier alijihakikishia taji kwa kunyakua mkondo wa 17 (Loldia2).

Ushindi huo uliweka Ogier juu ya jedwali kwa saa 3:11:54.6, sekunde 8.3 mbele ya Katsuta naye bingwa wa dunia mwaka 2019 Ott Tanak nyuma dakika moja na sekunde 18.

Kisha, Tanak (Hyundai) alishinda mkondo wa mwisho 18 wa Hell’s Gate2 maarufu Power Stage kupata alama zote tano za bonasi.

Ogier sasa anaongoza jedwali la WRC mwaka 2021 kwa alama 133 baada ya duru sita za kwanza kwenye ligi hiyo ya duru 12. Alizoa pointi 27 kwenye Safari Rally. Evans anasalia katika nafasi ya pili kwa alama 99 baada ya kujiongezea alama moja ya kumaliza nafasi ya 10 na pointi tatu za bonasi kwa kasi. Neuville yuko nafasi ya tatu kwa alama 77 baada ya kuambulia pakavu jana.

Tanak alijiongezea alama 20 muhimu kwa kukamata nafasi ya tatu Safari Rally na pia kupata bonasi ya alama tano kutokana na kasi ya juu katika mkondo wa mwisho wa Power katika eneo Hell’s Gate.

Raia huyo wa Estonia sasa ana alama 69. Katsuta alivuna alama 18 muhimu kwa kutamatisha Safari Rally katika nafasi ya pili. Ana jumla ya alama 66, pointi 10 mbele ya raia wa Finland, Kalle Rovanpera. Mfaransa Fourmaux pamoja na Muingereza Gus Greensmith wanafuatana katika nafasi ya saba na nane kwa alama 32, mtawalia.

Onkar anapatikana katika nafasi 15 kwa jumla kwa alama sita. Wakenya Karan Patel (alama nne) na mshindi wa mataji mengi ya Safari Rally yasiyo ya WRC, Carl Tundo wako katika nafasi ya 19 na 21 kwa alama nne na mbili, mtawalia.

You can share this post!

Drama washukiwa wa utekaji nyara wakinaswa

TAHARIRI: TSC sasa iheshimu uongozi wa KNUT