• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
NIMETIMIZA NDOTO: Kipchoge anyakua dhahabu ya marathon

NIMETIMIZA NDOTO: Kipchoge anyakua dhahabu ya marathon

Na MASHIRIKA

ELIUD Kipchoge amesema “ametimiza ndoto yake kitaaluma” baada ya kuwa mwanariadha wa kwanza tangu 1980 kuhifadhi dhahabu ya Olimpiki katika mbio za marathon nchini Japan.

Bingwa huyo wa dunia ambaye pia ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika marathon, alisajili muda wa saa 2:08.38 na kumpiku Abdi Nageeye wa Uholanzi kwa sekunde 80 zaidi.

Pengo hilo ndilo kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya washindi wawili wa kwanza wa marathon tangu Frank Shorter wa Amerika asajili muda wa saa 2:12.19 mbele ya Karel Lismont wa Ubelgiji (2:14.31) kwenye Olimpiki za Munich, Ujerumani mnamo 1972.

Bashiri Abdi wa Ubelgiji alizoa nishani ya shaba nchini Japan kwa saa 2:10.00 baada ya kumzidi ujanja Mkenya Lawrence Cherono (2:10.02). Amos Kipruto aliyekuwa mwakilishi mwingine wa Kenya, hakukamilisha mbio hizo zilizonogeshwa na wanariadha 106 kutoka mataifa 45.

Ushindi wa Kipchoge uliwezesha Kenya kukamilisha mashindano ya Olimpiki mwaka huu katika nafasi ya kwanza barani Afrika na ya 19 duniani. Kenya ilijizolea jumla ya medali 10 – nne za dhahabu, nne za fedha na mbili.

Kipchoge, 36, sasa ndiye binadamu wa tatu kuwahi kutetea kwa mafanikio dhahabu ya Olimpiki. Abebe Bikila wa Ethiopia (1960 Roma, 1964 Tokyo) na Mjerumani Waldemar Cierpinski (1976 Montreal, 1980 Moscow) ndio watimkaji wengine kuwahi kuhifadhi ufalme wa Olimpiki katika marathon.

“Nimetimiza ndoto yangu kwa kushinda marathon ya Olimpiki mara mbili mfululizo. Natazamia kuchochea kizazi kijacho kianze kuthamini michezo na kuamini kwamba hakuna kisichowezekana,” akatanguliza Kipchoge.

“Ndoto hii yangu imekuwa spesheli na imegharimu nidhamu na maandalizi makubwa. Katika michezo, kuna kushinda na kupoteza, lakini leo imekuwa siku yangu ya tija na fahari,” akasema.

Mbio hizo za kilomita 42 zilizoandaliwa katika mji wa Sapporo, zilimpa Kipchoge jukwaa la kujizolea medali ya nne ya Olimpiki.

Kipchoge aliwahi kushinda nishani ya shaba na fedha katika mbio za 5,000m kwenye Olimpiki za 2004 na 2008 jijini Athens na Beijing mtawalia. Ndiye binadamu wa kwanza kuwahi kukamilisha marathon chini ya saa mbili katika Ineos Challenge kwa saa 1:59.40 jijini Vienna, Austria 2019.

You can share this post!

DIMBA: Mwatate All Stars FC yapania kushinda taji

Madhara ya kutumia dawa bila ushauri wa daktari