• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
DIMBA: Mwatate All Stars FC yapania kushinda taji

DIMBA: Mwatate All Stars FC yapania kushinda taji

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MASHABIKI wa klabu ya Mwatate All Stars FC wanatekeleza jukumu kubwa la kuisaidia timu yao kutafuta msaada wa kugharamia safari za timu yao kwa mechi za ugenini.

Mashabiki hao wamekuwa wakitembea na fomu za kuwaomba wakazi wa mji huo wa Mwatate pamoja na wahisani kuisaidia timu kwa gharama za safarui zao za mechi wanazocheza nje ya mji wao huo.

Kwa wachezaji wa timu hiyo, wamepania kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye Ligi ya jimbo la Pwani wanayoshiriki mwaka huu lakini wanatarajia kuwania ushindi wa ligi hiyo msimu ujao wa 2021-2022.

Nahodha wa timu hiyo, John Terry Modibo amesema kuwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja unusu ambacho hawakucheza kutokana na marufuku ya serikali juu ya kujikinga na virusi vya corona, uliwaathiri kwani wengi wao hawakufanya mazoezi.

“Lakini tunajitahidi hivi sasa kuhakikisha tunarudia hali ya mchezo wetu ili tuweze kama si kushinda basi tumalize katika nafasi itakayowaridhisha mashabiki wetu,” akasema Modibo.

Anasema kuna umuhimu wa kuhakikisha wanafanya vizuri na hata kama hawatachukua taji msimu huu, watapigana kuhakikisha msimu ujao wanatekeleza lengo lao la kupanda ngazi hadi Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili.

Naibu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ekron Mwanyumba amesema wanapigana kujaribu kushinda ligi hiyo ama kujitahidi kuhakikisha wanakamilisha ligi hiyo katika nafasi nzuri.

“Niko katika harakati za kuunda wanasoka wenye vipaji ambao wengineo wanasubiriwa na klabu kadhaa za Supa Ligi ya Kitaifa msimu ujao. Wako vijana ambao nawaunda kuihami timu wakati wenzao watakaposajiliwa kwengineko,” akasema Mwanyumba.

Alimshukuru sana mwenyekiti wa klabu hiyo Boniface Mwabonje ambaye amekuwa akiwasaidia mara kwa mara katika kuigharamia timu na akaomba wadhamini wajitokeze ili waweze kukamilisha mechi zao hasa zile za ugenini ambazo ni za gharama kubwa.

Kikosi cha timu hiyo ya Mwatate All Stars kina John Modibo, Arnold Makau, Willybind Massawe, Michael Kombe, Michael Maganga, Michael Oloo, Louis Shuma, Hezron Mwandisha, Ganton Makumbi, Henderson Nyiro, Kelvin Mchana, Zuberi Mnyaka, Peter Mwadime, Anthony Masimbi na Antony Jumbe.

Naye katibu Mussa Toni anaamini kama wahisani watajitolea kuisaidia klabu, timu itaweza kupanda ngazi kwa kasi na kufikia pale walipo na nia ya kufika kwa Ligi Kuu ya Kenya. “Naamini tutaweza kufika huko kilele cha ligi za hapa nchini, tukiwa na udhamini imara,” akasema Toni.

Kinara Mwabonje naye pia ametoa wito kwa wahisani wajitokeze kuisadia klabu hiyo ambayo anaamini itawakilisha vizuri Mwatate. “Tunataka tufikie pale wenzetu wamefika na zaidi ya hapo ili vijana wetu wapate kuinua vipaji vitakavyowafaa maishani,” akasema.

Alieleza imani yake kuwa wana wachezaji wanaoweza kufikia viwango vya kuhitajika hata na klabu za ligi kuu ikiwa watapata motisha wa kuwa na vifaa vya kutosha vya mazoezi na mechi pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa wachezaji na klabu kuwa nayo.

Mwabonje anasema wana mipango kabambe ya kutaka kuyatekeleza yakiwemo ya kutaka kufanya ziara ya kutemebelea sehemu mbalimbali ya nchi wakati wa kumalizika kwa ligi lakini yote yatategemea kupatikana kwa fedha za kugharamia ziara hizo.

“Tunataka sana wachezaji wetu wacheze sehemu mbalimbali kwa ajili ya kupata uzoefu na hivyo ningeliomba wafadhili wajitokeze kutusaidia kufanikisha mipango tulonayo,” akasema.

You can share this post!

DIMBA: Kiganjo Kings wanatambua bidii ya mchwa itawajenga

NIMETIMIZA NDOTO: Kipchoge anyakua dhahabu ya marathon