• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
NYOTA WA WIKI: Marcus Rashford

NYOTA WA WIKI: Marcus Rashford

NA GEOFFREY ANENE

MARCUS Rashford ni mmoja wa wachezaji wanaosisimua mashabiki wa soka nje na ndani ya Uingereza, akivalia jezi nambari 10 kikosini Manchester United.

Ni mvamizi aliye moto wa kuotea mbali; kasi na chenga zake za maudhi zikidhalilisha makipa wa upinzani.

Katika mechi za hivi majuzi ugani Old Trafford, Rashford ameona lango Man-United ikipepeta Sheriff Tiraspol 3-0 mnamo Oktoba 27 katika kombe la Europa League; West Ham 1-0 mnamo Oktoba 30, Nottingham Forest 3-0 mnamo Desemba 27 na Bournemouth 3-0 mnamo Januari 3 katika michuano ya Ligi Kuu (EPL).

Vile vile, alilambisha sakafu makipa wakilemea Aston Villa 4-2 mnamo Novemba 10, Burnley 2-0 mnamo Desemba 21 na Charlton 3-0 mnamo Januari 10 katika Kombe la Carabao, na kutinga bao vigogo hao wakilima Everton 3-1 mnamo Januari 6 Kombe la FA.

Ukatili wake pia umemfanya apate magoli 18 katika mechi 30 msimu huu wa 2022-2023 yakiwemo saba kwenye EPL, manne katika Carabao, matatu ya Europa League na moja kwenye FA.

Mshambulizi huyo wa Uingereza alifungia taifa lake mabao matatu katika Kombe la Dunia lililokamilika Desemba 2022 jijini Doha, Qatar.

Rashford alienzi wavamizi stadi Ronaldo Luis Nazario de Lima kutoka Brazil na Mreno Cristiano Ronaldo tangu utotoni.

Alianza soka akiwa shuleni wakati huo akiwa na umri wa miaka mitano.

Amechezea Manchester United, maarufu Red Devils, maisha yake yote baada ya kuingia akademia ya klabu hiyo na kusaini kandarasi akiwa na umri wa miaka saba.

Mara ya kwanza alifanikiwa kuitwa kikosi cha kwanza cha watu wazima cha Man-United ilikuwa 2015 akiwa miaka 18.

Alipewa nafasi ya kuanza mechi kwa mara ya kwanza 2016 dhidi ya Midtjylland katika kombe la Europa League, na hakuchukua muda kufungua ukurasa wa magoli kwani alipepeta mawili katika mchuano huo.

Kisha akatinga bao la pekee Red Devils walipofinya majirani wao Manchester City.

Grafu ya Rashford imekuwa ikipanda na kushuka, ingawa sasa ni fowadi tegemeo kambini Old Trafford baada ya nyota Ronaldo kuondoka mwezi Desemba.

Alipata fursa ya kuvalia jezi maarufu ya nambari 10 msimu 2018-2019 baada ya gunge Zlatan Ibrahimovic wa Uswidi kuhama klabu.

Ni msimu huo ambapo Rashford aliitwa katika timu ya taifa ya watu wazima ya Uingereza – Three Lions – kwa mara ya kwanza.

Alifungua akaunti yake ya kimataifa dhidi ya Slovakia katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia lsa 2018 nchini Urusi.

Akiwa na umri wa miaka 25 pekee, muda utakuwa msema kweli kama atawafikia washambulizi matata Ruud van Nistelrooy na Wayne Rooney waliovalia jezi nambari 10 ugani Old Trafford kabla ya kustaafu.

Atafikia rekodi ya Dennis Viollet akifunga katika mechi ya tisa mfululizo za nyumbani, wakati Man-United imealika mabingwa watetezi Manchester City kwenye gozi la EPL, leo Jumamosi.

  • Tags

You can share this post!

Kaunti za Pwani zenye raslimali kunufaika pendekezo la...

STAA WA SPOTI: Huyu hapa malkia wa uendeshaji baiskeli Kenya

T L