• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Okutoyi aingia robo-fainali ya mashindano ya tenisi ya JB2 Sousse nchini Tunisia

Okutoyi aingia robo-fainali ya mashindano ya tenisi ya JB2 Sousse nchini Tunisia

Na GEOFFREY ANENE

MWANATENISI Angella Okutoyi ametinga robo-fainali ya mashindano ya Afrika ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 maarufu kama JB2 Sousse nchini Tunisia mnamo Jumanne.

Okutoyi, ambaye ni Mkenya pekee aliyesalia katika vita vya kuwania taji baada ya kinadada wenzake Cynthia Wanjala, Alicia Owegi na Roselida Asumwa na wavulana Derick Ominde na Kael Shah kubanduliwa katika raundi ya kwanza Novemba 22, amebwaga Meriem Ezzedine. Amelemea Mtunisia huyo kwa seti mbili kavu za 6-2, 6-1.

Okutoyi, ambaye alipata tiketi ya bwerere ya raundi ya 32-bora kabla ya kuzaba Ezzedine katika raundi ya 16-bora, atakabiliana na Ekua Youri kutoka Botswana kwenye robo-fainali hapo Jumatano.

Youri ameduwaza Rufaro Magarira (Zimbabwe) na Sara Akid (Morocco) katika raundi mbili za kwanza mtawalia kwa hivyo hatarajiwi kuwa mpinzani rahisi. Owegi, Wanjala na Asumwa walibanduliwa na Naledi Raguin (Botswana), Tanyaradzwa Midzi (Zimbabwe) na Amira Bargaoui (Tunisia) mtawalia.

Okutoyi anaorodheshwa wa pili katika mashindano haya. Anakamata nafasi ya 142 kwenye viwango bora vya chipukizi vya Shirikisho la Tenisi Duniani (ITF). Youri ni nambari 849, Ezzedine (1,277), Magarira (315) na Akid (530).

You can share this post!

Mzozo wa urithi wa kisiasa Nandi watishia nafasi ya Sang...

CHARLES WASONGA: Njama ya kuua OKA itagharimu Wakenya

T L