• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
CHARLES WASONGA: Njama ya kuua OKA itagharimu Wakenya

CHARLES WASONGA: Njama ya kuua OKA itagharimu Wakenya

Na CHARLES WASONGA

NINAKERWA na ripoti kwamba mirengo ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga inapanga kuunda miungano miwili mikuu kwa kusambaratisha muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Kwanza, hatua hiyo inakwenda kinyume na misingi ya demokrasia kwani inalenga kuendeleza dhana kwamba kinyang’anyiro cha urais ni kati ya “farasi wawili”, Dkt Ruto na Bw Odinga.Kwa muda mrefu imeaminika kuwa Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiwarai vinara wa OKA;

Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu) wamuunge mkono Bw Odinga.Lengo lake ni kuunda muungano mkubwa ukiongozwa na Bw Odinga, kusudi kuzima ndoto ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022.

Ni wazi kuwa ili kuunda muungano kama huo, Rais Kenyatta na Bw Odinga, watalazimika kuwaahidi vinara hao nyadhifa mbalimbali serikalini ikizingatiwa kuwa siasa ni mchezo wa “nipe nikupe”.Hii ina maana kuwa ili kuwafaa vinara hao wa OKA, Bw Odinga atalazimika kubuni nyadhifa zaidi serikalini endapo ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa sababu mchakato wa mageuzi ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) uliobuni nyadhifa zaidi katika safu ya juu ya uongozi nchini ulizimwa na mahakama, Odinga atatumia mamlaka ya urais kubuni nyadhifa zaidi katika baraza la mawaziri.Katika utawala wake, Rais Kenyatta amefanya hivyo kwa kubuni vyeo vya mawaziri wasaidizi (CAS), Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri kuhusu Utekelezaji na Ushirikishi wa Majukumu ya Serikali inayoshikiliwa na Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i.

Hali itakuwa sawa na hiyo endapo mrengo wa Dkt Ruto utafaulu kuvutia baadhi ya vinara wa OKA upande wake.Licha ya Dkt Ruto kushikilia kuwa chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakina mipango ya kubuni miungano na vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, Seneta wa Tharaka Nithi Prof Kithure Kindiki amethibitisha kuwa watahitaji kuunda muungano kuanzia Februari mwaka ujao ili kuboresha nafasi yao ya kushinda urais.

Duru zimeeleza kuwa Dkt Ruto anapania kushirikiana na Bw Mudavadi au Bw Musyoka baada ya Seneta Moi kuonyesha dalili za wazi wazi kwamba anaegemea mrengo wa handisheki, wake Rais Kenyatta na Bw Odinga.Kwa upande mwingine, wandani wa Bw Odinga wamethibitisha kuwa Mbw Odinga na Musyoka wanafanya mazungumzo ya siri kwa lengo la kufanya kazi pamoja kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Seneta Moi pia ameshirikishwa katika mazungumzo hayo.Kimsingi, mipango hii ya kugawanywa kwa vinara wa OKA ili kuwe na wagombeaji wawili wakuu2022, itawavunja moyo baadhi ya Wakenya wanaopanga kupigia kura wagombeaji urais wengine mbalina Dkt Ruto na Bw Odinga.

Hali kama hii huenda ikachangia wapigakura wasiokumbatia sera za Ruto na Raila kususia uchaguzi mkuu ujao. kwa kuhisi kunyimwa ‘haki’ ya kuamua mgombeaji urais wanayemtaka, kuambatana kipengele cha 38 cha Katiba.

Vile vile, miungano miwili mikuu kinzani itakayobuniwa na mirengo ya Dkt Ruto na Bw Odinga utakuwa mzigo mkubwa kwa walipa ushuru kwa kuunda nyadhifa zaidi katika serikali ijayo endapo mmoja wao ataibuka mshindi.

Ukweli ni kwamba atakayeshika usukani baada ya Rais Kenyatta kustaafu, atarithi mzigo mkubwa wa madeni wa karibu Sh9 trilioni. Ili kulipa madeni haya na kugharamia mahitaji ya nyadhifa zaidi zitakazobuniwa kukidhi mahitaji ya wanasiasa, serikali ijayo italazimika kuongeza ushuru kwa bidhaa mbalimbali, hali itakayowaumiza Wakenya hata zaidi.

You can share this post!

Okutoyi aingia robo-fainali ya mashindano ya tenisi ya JB2...

Gavana Mvurya asifiwa kufadhili klabu za Kwale

T L