• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Okutoyi atinga nusu-fainali ya tenisi ya J3 nchini Misri

Okutoyi atinga nusu-fainali ya tenisi ya J3 nchini Misri

Na GEOFFREY ANENE

MWANATENISI Angella Okutoyi ametinga nusu-fainali ya mashindano ya kwanza ya daraja ya tatu ya J3 Cairo baada ya kulemea Briana Szabo kutoka Romania kwa seti 2-1 nchini Misri mnamo Agosti 25.

Okutoyi, 17, ambaye anaorodheshwa nafasi ya 188 duniani, alianza mchuano huo kwa kupoteza seti ya kwanza kwa alama 6-4 kabla ya kuzidia mchezaji huyo nambari 544 duniani seti mbili zilizofuata kwa alama 6-3, 6-0.

Briana,15, hakuwa mpinzani rahisi kwa sababu alikuwa amebandua mchezaji anayeorodheshwa juu katika mashindano hayo Juliette Bovy kutoka Ubelgiji (169 duniani) kwa seti 2-0 za alama 6-4, 6-2 katika raundi ya pili.

Okutoyi, ambaye alipata nafasi yake bora duniani ya 127 aliposhinda mashindano mawili jijini Nairobi mapema 2021 kabla ya kurushwa hadi 198, alianza mashindano ya pili ya Cairo kwa kupepeta mwenyeji Maria Charl (nambari 241 duniani) 6-0, 6-1 katika randi ya kwanza. Kisha, alicharaza Mmisri mwingine Jermine Sherif (256 duniani) 6-4, 6-3 katika raundi ya pili. Briana alichapa Mmisri Mariam Ibrahim 6-3, 7-6 katika raundi ya kwanza.

Okutoyi atalimana na nambari 195 duniani Mbrazil Ana Candiotto katika nusu-fainali hapo Agosti 26.

Mkenya huyo alipoteza dhidi ya Sherif katika robo-fainali ya mashindano ya kwanza ya J3 Cairo yaliyokamilika Agosti 20.

You can share this post!

Wito viongozi wa Mlima Kenya wajipange wawe pamoja kisauti

Serikali kutumia vijana na wanabodaboda kuendesha kampeni...