• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Omanyala azamia zoezi kuelekea Italia, Czech

Omanyala azamia zoezi kuelekea Italia, Czech

Na GEOFFREY ANENE

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala, ameimarisha mazoezi tayari kuelekea Bara Ulaya kwa mashindano mawili kabla ya Riadha za Afrika nchini Mauritius.

Bingwa huyo mpya wa Kip Keino Classic anasema kuwa atashiriki mbio za kimataifa za Castiglione della Pescaia nchini Italia mnamo Mei 22 halafu Ostrava Golden Spike nchini Czech mnamo Mei 31.

“Msimu huu umejaa mashindano kwa hivyo muda wa kupumzika ni mchache sana. Nimesharejea mazoezini,” alieleza Taifa Leo.

Omanyala alitetemesha kwenye makala ya tatu ya Kip Keino alipotwaa taji mbele ya maelfu wa mashabiki akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, kwa muda bora mwaka huu wa sekunde 9.85. Aliduwaza Waamerika Fred Kerley (9.92) na Isiah Young (10.13) walioridhika na nafasi ya pili na tatu, mtawalia.

Kerley alikuwa ameshinda Omanyala mara mbili katika Olimpiki 2020 jijini Tokyo, Japan mwaka jana akinyakua nishani ya fedha.

Omanyala,26, hakupata kupimana ubabe na bingwa wa Olimpiki Marcell Jacobs.

Mwitaliano Jacobs alipata matatizo ya kuumwa na tumbo na kutibiwa katika hospitali ya Ruaraka Uhai Neema, Nairobi.

Omanyala anayejivunia rekodi ya Afrika mbio za mita 100 ya sekunde 9.77, alitembelea Jacobs katika hospitali hiyo Jumapili.

Riadha za Afrika ni Juni 8-12.

  • Tags

You can share this post!

Raila atuliza vita vya ndani katika Azimio

Ruto ajitetea katika kesi ya kushinikiza apokonywe wadhifa

T L