• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
Omanyala bado hajapata ruhusa kuenda Amerika Riadha za Dunia

Omanyala bado hajapata ruhusa kuenda Amerika Riadha za Dunia

Na AYUMBA AYODI

BINGWA wa Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala ni miongoni mwa wanariadha sita ambao bado wanahangaika kupata ruhusa ya kusafiri hadi Amerika kushiriki Riadha za Dunia zinazoanza Julai 15 mjini Oregon.

Huku timu hiyo ikipokea baraka kutoka Ikulu jijini Nairobi, viongozi wa timu hiyo walikuwa wamekaba Waziri wa Michezo Amina Mohamed awasaidie kupata visa.

Timu hiyo iliratibiwa kusafiri kwa vikundi viwili mnamo Jumatatu na Jumanne usiku.

Kundi la kwanza la watu 23, ambalo lilijumuisha wanariadha 19, lilisafiri Jumatatu usiku likitumia ndege tatu tofauti za kampuni ya Qatar Airways, KLM Royal Dutch Airlines na Lufthansa Airlines.

Omanyala, ambaye anashikilia rekodi ya Afrika mita 100 ya sekunde 9.77, pamoja na meneja wa timu Rono Bunei na wataalamu wote watatu wa kunyoosha misuli wa timu ya Kenya Jessica Shiraku, John Muraya na Japheth Kariakim, hawakuwa wamepokea ruhusa hiyo.

Timu ya Kenya haikuwa imesafiri na daktari yeyote kwani daktari wa timu Victor Bargoria alipangiwa kuelekea Amerika mnamo Juni 12 jioni.

Rais Uhuru Kenyatta alipatia bendera ya Kenya nahodha wa timu, Julius Yego, ambaye ni bingwa wa dunia kurusha mkuki mwaka 2015, pamoja na nahodha msaidizi Omanyala.

Bunei alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa huku timu hiyo ikifika katika Ikulu kupewa bendera.

“Inasababisha hofu, hasa kwa sababu mashindano yataanza Ijumaa na tuna ndege tutakazotumia kutoka mataifa mengine ili kufika mwisho wa safari,” alisema Bunei na kuongeza kuwa mambo yatakuwa magumu kwa Omanyala atakayeanza kampeni Ijumaa kabla ya fainali Jumamosi.

Omanyala alisema kuwa ana matumaini kuwa atafanikiwa kusafiri huku Rais Kenyatta akiahidi kusafiri hadi mjini Birmingham, Uingereza kumtazama akitifua vumbi kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Julai 28 hadi Agosti 9. Raundi mbili za kwanza za mita 100 wanaume mjini Oregon ni Julai 15 kabla ya nusu-fainali na fainali Julai 16.

Bunei alieleza kuwa baadhi ya wanariadha ambao hawakuwa na tiketi wako na visa tayari, lakini wanashirikiana na wizara kutatua suala hilo.

“Mmoja wa wanariadha hao ni Kumaru Taki katika mbio za mita 1,500,” alisema Bunei.

Wanariadha walioratibiwa kuabiri ndege ya kuelekea Amerika mnamo Julai 12 ni bingwa wa Olimpiki mita 800 Emmanuel Korir, mtimkaji wa mbio za mita 400 kuruka viunzi Moitalel Mpoke, mkimbiaji wa mita 3,000 kuruka viunzi na maji Abraham Kibiwott na mtimkaji wa mita 1,500 Edinah Jebitok.

Kocha wa fani ya kutembea haraka George Kariuki na daktari Bargoria pia waliratibiwa kusafiri Jumanne.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Raila apuuza migogoro ndani ya Azimio Taita Taveta

BORESHA AFYA: Vyakula vya kuongeza nguvu za kiume

T L