• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Oyoo ajaza nafasi ya nahodha Amonde, Simiyu pia ajumuisha wachezaji 5 wapya

Oyoo ajaza nafasi ya nahodha Amonde, Simiyu pia ajumuisha wachezaji 5 wapya

Na GEOFFREY ANENE

NELSON Oyoo amechukua majukumu ya nahodha wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande kutoka kwa Andrew Amonde aliyestaafu baada ya Olimpiki mnamo Agosti.

Oyoo ataongoza Kenya Shujaa msimu huu kwenye Raga za Dunia 2021 jijini Vancouver (Septemba 18-19), Edmonton (Septemba 25-26), Singapore (Oktoba 29-20), Dubai (Desemba 3-4) na Cape Town (Desemba 10-12).

Kocha Mkuu wa Kenya Shujaa, Innocent “Namcos” Simiyu alieleza Taifa Leo hapo Septemba 10 kuwa Oyoo alichaguliwa kutumikia timu katika wadhifa huo baada ya “kuangalia uongozi wake mzuri ndani na nje ya uwanja pia maadili na tabia yake”.

Jeffrey Oluoch kutoka klabu ya Homeboyz atakuwa naibu wa mchezaji huyo wa klabu ya Top Fry Nakuru.

Kikosi cha Shujaa kitakachoekelea nchini Canada hapo Septemba 13 kina wachezaji watano wapya – Levi Amunga, Derrick Keyoga, Alvin Marube, Mark Kwemoi na Timothy Mmasi.

“Tumekuwa na juma moja la kambi ya mazoezi ya hali ya juu katika klabu ya michezo ya Parklands na vijana wamefaulu kufikia malengo yao. Tuna hamu kubwa tunapoelekea Vancouver,” alisema na kufichua kuwa uamuzi wa kujaribu wachezaji wapya ni kutupia jicho mashindano ya Jumuiya ya Madola na Kombe la Dunia mwaka 2022.

“Lengo letu ni kuanza duru za Vancouver na Edmonton kwa kishindo. Tukifaulu kufika robo-fainali na nusu-fainali, basi itakuwa kitu kikubwa kwetu katika safari yetu ya mashindano ya Jumuiya ya Madola na Kombe la Dunia. Shujaa itakamilisha matayarisho yake hii leo.

Kikosi cha Shujaa: Nelson Oyoo (Nakuru, nahodha), Jeffrey Oluoch (Homeboyz, nahodha msaidizi), Alvin Otieno (Homeboyz), Timothy Mmasi (MMUST), Herman Humwa (Kenya Harlequin), Harold Anduvati (Menengai Oilers), Willy Ambaka (Narvskaya Zastava, Urusi), Daniel Taabu (Mwamba), Mark Kwemoi (Menengai Oilers), Levi Amunga (KCB), Billy Odhiambo (Mwamba), Derrick Keyoga (Menengai Oilers), Alvin Marube (Impala Saracens).

You can share this post!

GUMZO LA SPOTI: Real Madrid yapanga usajili wa nguvu kwenye...

Rais wa Estonia ajiunga na Wakenya kwenye mbio katika msitu...