• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Palace wafunga mawili na kuendeleza masaibu ya Sheffield United mkiani mwa jedwali la EPL

Palace wafunga mawili na kuendeleza masaibu ya Sheffield United mkiani mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

FOWADI Eberechi Eze alitokea benchi na kufungia Crystal Palace bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kusaidia waajiri wake kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Sheffield United ambao kwa sasa wanavuta mkia kwa alama mbili pekee baada ya mechi 17 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Jeffrey Schlupp aliwafungulia Palace ukurasa wa mabao katika dakika ya nne kabla ya nyota huyo raia wa Ghana kuondolewa uwanjani kwa sababu ya jeraha katika mechi hiyo iliyochezewa ugani Selhurst Park.

Kutolewa kwa Schlupp kulimpisha Eze aliyeingia ugani kwa matao ya juu. Fowadi huyo wa zamani wa Queens Park Rangers (QPR) alipata mpira katika nusu ya pili ya uwanja na kukimbia nao hadi hatua ya mita 18 kutokana langoni mwa Sheffield United kisha kuachilia fataki iliyoja wavuni.

Sheffield United ya kocha Chris Wilder ilisalia butu katika safu ya mbele na kushindwa kupiga Palace katika mchuano wao wa 17 ligini msimu huu, waliweka rekodi ya kikosi ambacho kimekosa kushinda mechi ya EPL kwa muda mrefu zaidi ligini.

Sheffield United almaarufu The Blades walikamilisha mechi wakijivunia maarifa ya chipukizi Antwoine Hackford, 16, aliyeweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa na kikosi hicho katika EPL.

Chini ya kocha Roy Hodgson, Palace waliingia ugani kwa ajili ya mechi hiyo wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi baada ya kupiga msururu wa mechi tano za awali bila mafanikio.

Eze, 22, ameelewa haraka mfumo wa mchezo kambini mwa Palace waliomtwaa kutoka QPR kwa mkataba wa miaka mitano uliogharimu Sh2.7 bilioni mnamo Agosti 2020.

Bao la kwanza la Eze lilikuwa dhidi ya Leeds United mnamo Novemba 2020. Wilder alikuwa mwingi wa hasira mwishoni mwa mchuano huo huku akiwalaumu pakubwa wanasoka wake kwa utepetevu uliompa Eze ambaye ni chipukizi wa zamani wa Arsenal fursa ya kuwatatiza pakubwa katika safu ya ulinzi.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Palace kukamilisha mechi bila ya kufungwa bao katika EPL msimu huu na ni matarajio ya Hodgson kwamba ushindi huo utawaondolea vijana wake maruerue ya vichapo vinono vya 7-0 na 3-0 kutoka kwa Liverpool na Aston Villa mtawalia katika mechi mbili za awali.

Japo Palace wamerejea katika uthabiti wao wa awali wa kushinda mechi, huenda kikosi hicho kikakabiliwa na pigo la kuagana na fowadi mahiri raia wa Ivory Coast, Wilfried Zaha ambaye kwa sasa anawaniwa pakubwa na Paris Saint-Germain (PSG) na AC Milan nchini Ufaransa na Italia mtawalia. Zaha ndiye alichangia bao la kwanza ambalo Palace walifungiwa na Schlupp.

Alishirikiana pakubwa na Christian Benteke aliyeondolewa baadaye uwanjani kutokana na jeraha.

Palace kwa sasa wanajiandaa kwa mechi ngumu za ugenini zitakazowakutanisha na Wolves katika Kombe la FA kabla ya kuvaana na Arsenal na Manchester City kwa usanjari huo katika michuano miwili ya EPL ugani Emirates na Etihad mtawalia. Kwa upande wao, Sheffield United watakuwa wageni wa Bristol Rovers katika raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 9, 2021.

  • Tags

You can share this post!

Brighton watoka nyuma kwa mabao 3-1 na kulazimisha sare ya...

PSG wamwajiri kocha Pochettino kwa mkataba wa miezi 18