• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Brighton watoka nyuma kwa mabao 3-1 na kulazimisha sare ya 3-3 dhidi ya Wolves ligini

Brighton watoka nyuma kwa mabao 3-1 na kulazimisha sare ya 3-3 dhidi ya Wolves ligini

Na MASHIRIKA

LEWIS Dunk alisaidia waajiri wake Brighton kutoka nyuma kwa mabao 3-1 na kuwalazimishia Wolves sare ya 3-3 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliosakatiwa ugani Amex mnamo Jumamosi.

Matokoeo hayo yaliwasaza Brighton almaarufu The Seagulls katika nafasi ya 17 kwa alama 14, tatu pekee nje ya mduara unaojumuisha vikosi vilivyopo katika hatari ya kuteremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za msimu huu.

Hata hivyo, kujituma kwa Brighton kunatarajiwa kuwapa motisha zaidi ikizingatiwa kwamba wameshinda mechi moja pekee kutokana na 15 zilizopita.

Aaron Connolly aliwafungulia Brighton ukurasa wa mabao katika dakika ya 13 baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi aliyopokezwa na Leandro Trossard. Hata hivyo, juhudi zake zilifutwa na Romain Saiss aliyemwacha hoi kipa Robert Sanchez baada ya kufunga kwa kichwa krosi aliyomegewa na beki wa zamani wa Barcelona, Nelson Semedo katika dakika ya 19.

Brighton waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo walijipata chini kwa mabao 2-1 baada ya Dan Burn kujifunga licha ya kipa Sanchez kujitahidi na kupangua kombora alilovurmishiwa na Pedro Neto.

Burn alikamilisha kipindi cha kwanza kwa masaibu zaidi alipomchezea visivyo fowadi Adama Traore ndani ya kijisanduku na kusababisha penalti iliyojazwa kimiani na Ruben Neves katika dakika ya 44. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Neves kufungia Wolves tangu Februari 2020.

Brighton walianza kipindi cha pili kwa matao ya juu na wakafunga bao la pili lililowarejesha mchezoni katika dakika ya 46 kupitia penalti iliyochanjwa na fowadi raia wa Ufaransa, Neal Maupay aliyechezewa visivyo na Joao Moutinho ndani ya eneo la hatari.

Bao hilo liliwapa Brighton ari ya kuvamia zaidi lango la Wolves na presha kutoka kwa Adam Webster ilimwezesha Dunk kufunga bao la tatu kutokana na krosi ya Trossard katika dakika ya 70.

Wolves kwa sasa wanajiandaa kuwa wenyeji wa Crystal Palace kwenye mchuano wa raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 8 huku Brighton wakiwaendea Newport County ya Ligi ya Daraja la Pili mnamo Januari 10.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal watangaza rasmi ufufuo wao ligini kwa kupokeza West...

Palace wafunga mawili na kuendeleza masaibu ya Sheffield...