• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Pele azikwa kishujaa nje kidogo ya uwanja wa Santos

Pele azikwa kishujaa nje kidogo ya uwanja wa Santos

JOHN ASHIHUNDU Na MASHIRIKA

GWIJI wa soka, Edson Arantes do Nascimento, maarufu kama Pele amezikwa leo Jumanne kishujaa nje kidogo ya uwanja wa Santos alikoanzia kucheza akiwa na umri wa miaka 15.

Rais mpya wa Brazil, Luiz Inacio Lula da Silva ni miongoni mwa waombolezaji waliotoa heshima zao za mwisho kwa gwiji huyo ugani Santos Stadium.

Marehemu aliyeweka historia kwa kutwaa Kombe la Dunia mara tatu aliaga dunia hospitalini mjini Sao Pualo Alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 82.

Baada ya hafla za uwanjani, hatimaye msafara ulizunguka mitaani kwenye barabara ya Santos, kabla ya maziko maalum yaliyohudhuriwa na jamii na marafiki wachache kwenya gorofa ya vyumba 32 ya Memorial Necropole Ecumenica, ambayo tayari yanahifadhi makaburi 1600.

Serikali ya Brazil ilitangaza siku tatu za kuomboleza mkongwe huyo ambaye amekuwa akipokea matibabu tangu 2021, akiugua saratani ya utumbo mpana kwa muda mrefu.

Rais wa FIFA, Gianni Infantino alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria misa ya wafu iliyofanyika Jumatatu.

Maelfu ya mashabiki wa soka walimiminika barabarani huku gari lililobeba jeneza la mwili wake likipelekwa uwanjani kwa heshima za mwisho.

Aliyekuwa kiungo mahiri wa Brazil Ze Roberto na mwanaye Pele Eldinho walisaidia katika kubeba jeneza hilo, huku rambi rambi zikiendelea kutumwa na wazchezaji wa zamani pamoja na wa sasa Neymar na Vinicius Junior wakiendelea kutoka risala zao.

Kulikuwa na majonzi kwa wingi kutoka kwa mashabiki, huku wengine wakianguka sakafuni kumkumbuka Pele ambaye aliiletea nchi yake sifa tele za kimataifa kutokana na mafanikio yake uwanjani.

“Nilipata fursa ya kumuona akicheza soka mara kadhaa,” Joao Paulo Mchado, mkazi wa Santos aliambia mwandishi wa BBC, Katy Watson.

“Pele alikuwa balozi nambari moja wa taifa hili duniani, kulingana na maoni yangu. Ukizuru nchi, kitu cha kwanza watu kusema ni: Unatoka nchi ya Pele.”

Aliyekuwa rais wa klabu ya Santos, Marcelo Teixeira alisema Pele alikuwa “binadamu wa kipekee”.

Aliongeza: “Ni mtu aliyekuwa mkarimu, aliyejali maisha ya wengine, mbali na kuwa mnyenyekevu.”

Marcelo Buono, mzaliwa wa Santos anayeishi Miami ni miongoni mwa watu waliorejea nyumbani kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.

Wilson Genio na mtoto wake Miguel mwenye umri wa miaka 13 ni miongoni mwa waombolezaji waliofika mapema kupiga foleni ugani Santos, huku akibeba maua mkonpono.

Sogora huyo aliyesaidia Brazil kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia mara tatu mnamo 1958, 1962 na 1970 aliaga dunia Disemba 29 akiwa na umri wa miaka 82.

Pele alianza kuchezea timu kadhaa za mtaa akiwa mtoto mdogo, mbali na kuongoza kuongoza kikosi cha Bauru Athletico kwenye mashindano matatu ya vijana ya Serikali, akijidhihirisha kama talanta angavu.

Mnamo 1956, kocha wake, Waldemar de Brito alimpeleka hadi jiji la banadari la Santos kufanya majaribio katika klabu ya Santos, ambayo ilikuwa ya kulipwa.

Pale majaribioni, wakufunzi waliokuwa walikubaliana na kipaji chake, huku baadhi yao wakimuona kama mchezaji ambaye atakuwa bora zaidi duniani, wakati huo akiwa na umri wa miaka 15 tu.

Mwaka mmoja baadaye, Pele alipelekwa kwa timu kuu ya Santos na akafunga bao moja katika mechi yake ya kwanza. Kwa haraka, Pele aliibuka mfungaji bora ligini.

Miezi 10 baadaye, aliitwa kujiunga na timu ya taifa ya Brazil kutokana na kipaji chake cha hali ya juu, licha ya umri wake mdogo.

Pele alifunga bao lake la kimataifa akiwa na umri wa miaka 16, bao ambalo lilimfanya kuwa mchezaji mdogo zaidi kufunga katika mechi ya kimataifa.

Katika ngazi ya kimataifa, Pele aliisaidia Santos kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Sao Paulo mnamo 1958, na kumaliza msimu kama mfungaji bora.

Juhudi za kujiunga na klabu tajiri zikiwemo Manchester United na Real Madrid kumsajili alipokuwa bora zaidi duniani ziliambulia patupu baada ya Serikali ya Brazil kumtangaza “Hazina ya Kitaifa” ili kumzuia kuondoka nchini.

Mechi yake ya mwisho kuchezea Brazil ilikuwa 1971 dhidi ya Yugoslavo, kabla ya kustaafua rasmi kuchezea nchi yake 1974.

Akiendelea kusakata soka ya klabu, Pele aliamua kuyoyomea Amerika miaka miwili baadaye na kujiunga na klabu ya New York Cosmos, ambapo jina lake pekee liliinua kandanda nchini humo.

Mbali nausakataji soka, Pele alikuwa muigizaji, huku akiwa na mikataba kadhaa ya udhamini, huku jina lake likiendelea kung’ara ulimwenguni.

Mnamo 1992, aliteuliwa kuwa Balozi wa Umoja wa Mataifa na baadaye akafanywa Balozi Mwema wa UNESCO, kabla ya kuteuliwa Waziri wa Michezo na rais Fernando Henrique Cardoso mnamo 1995. Akitumia uwezo wake, Pele alipigana vikali na rushwa katika soka nchini Brazil.

Atakumbukwa kwa kuchangia pakubwa katika ombi la mafanikio la Rio de Janeiro kuwa waandalizi wa Michezo ya Olimpiki ya 2016, baada ya kuonekana kwenye sherehe za kufunga rasmi Michezo ya London 2012.

  • Tags

You can share this post!

Shirika la HESPO lafadhili wanamichezo, wasanii na kuvutia...

Mwanaume adaiwa kunyofolewa nyeti na mkewe kufuatia ugomvi

T L