• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Pigo KCB viongozi Tusker wakifungua mwanya wa alama tatu kileleni KPL

Pigo KCB viongozi Tusker wakifungua mwanya wa alama tatu kileleni KPL

Na CECIL ODONGO

KLABU ya KCB Ijumaa ilipata pigo katika juhudi za kushinda taji lake la kwanza kabisa la Ligi Kuu Nchini (KPL), ilipolemewa 2-1 na Vihiga United inayoning’inia kuteremshwa ngazi, katika uga wa Mumias Complex, Kaunti ya Kakamega.

Nao wapinzani wao wa karibu Tusker walifungua mwanya wa alama tatu kileleni kwa kuipiga Kakamega Homeboyz 2-0, zikiwa zimesalia mechi mbili pekee msimu huu utamatike.

Katika mechi nyingine mfungaji bora ligini Eric Kapaito alipepeta magoli mawili na kuchangia moja Kariobangi Sharks ikilemea Nzoia Sugar 3-1 uga wa kaunti ndogo ya Thika.

Hillary Simiyu alifungia Nzoia bao la kufutia machozi dakika ya 81 huku Peter Lwasa akiongeza la tatu kwa Sharks zikiwa zimesalia dakika mbili kipenga cha mwisho kilie.

Kapaito sasa ametikisa nyavu mara 24 na yuko kifua mbele kutwaa kiatu cha dhahabu, ikizingatiwa namba mbili ni Elvis Rupia wa AFC Leopards aliye na mabao 16.

Sharks ilipanda hadi nafasi ya nne kwa alama 47 huku Nzoia ikiwa nambari 14 kwa alama 29 baada ya mechi za raundi ya 30.

Kufuatia kichapo cha Ijumaa KCB ilisalia namba mbili kwa alama 58, tatu nyuma ya vinara Tusker ligi inapoelekea ukingoni.

Vihiga, ambao wangeshushwa ngazi iwapo wangepigwa Ijumaa, sasa wana pointi 23; moja mbele ya wavutamkia Western Stima ambao haikuwa na mechi wikendi hii.

Nayo Mathare United, inayocheza ugenini dhidi ya Bandari hii leo, ikiwa na alama 24.

Mabao ya Vihiga yalifungwa na Lawrence Luvanda na Stewart Omondi dakika za 16 na 34 baada ya Samuel Mwangi kuipa KCB uongozi dakika ya 14.

Tusker nayo ilipata mabao yake kupitia bao la kujifunga la Brian Eshihanda dakika ya 38 kisha Mike Madoya akaongeza la pili dakika ya 40.

Kutokana na kichapo hicho Homeboyz imeteremka hadi nafasi ya saba kwa alama 43.

You can share this post!

Hospitali yakiri kulemewa na wagonjwa wa corona

Vigogo Man-U, Chelsea na Liverpool mawindoni leo