• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
PSG watinga fainali ya French Cup baada ya kudengua Montpellier kupitia mikwaju ya penalti

PSG watinga fainali ya French Cup baada ya kudengua Montpellier kupitia mikwaju ya penalti

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) walitinga fainali ya French Cup msimu huu baada ya kuwapiku Montpellier kwa magoli 6-5 kupitia penalti kwenye nusu-fainali mnamo Mei 12, 2021.

Moise Kean alifungia PSG penalti ya ushindi baada ya Junior Sambia wa Montpellier kupaisha mkwaju wake juu ya mwamba wa goli la PSG.

Awali, Kylian Mbappe alikuwa amewaweka PSG kifua mbele katika dakika ya 10 kabla ya Gaetan Laborde kusawazishia Montpellier mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ingawa Mbappe aliwarejesha PSG uongozini katika dakika ya 50, juhudi zake zilifutwa na Andy Delort aliyefanya mambo kuwa 2-2 katika dakika ya 83 na kuhakikisha kwamba mshindi wa gozi hilo anaamuliwa kupitia penalti.

Fainali ya French Cup muhula huu itaandaliwa ugani Stade de France mnamo Mei 19 ambapo PSG watakutana na mshindi kati ya AS Monaco ambao ni washindani wao kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) au Vallieres wanaoshiriki Ligi ya Daraja la Nne.

Ushindi wa PSG dhidi ya Montpellier uliweka hai matumaini ya kocha Mauricio Pochettino kushindia PSG mataji mawili katika msimu wake wa kwanza kambini mwa kikosi hicho japo viongozi wa jedwali Lille wanapigiwa upatu wa kutia kapuni taji la Ligue 1.

Kufikia sasa, Lille wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama tatu zaidi kuliko PSG huku zikisalia mechi mbili pekee kwa kampeni za Ligue 1 msimu huu kutamatika rasmi.

Pochettino ambaye ni kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur aliaminiwa mnamo Januari 2021 kuwa mrithi wa kocha Thomas Tuchel ambaye kwa sasa anawatia makali masogora wa Chelsea. Pochettino alipanga kikosi chake cha kwanza dhidi ya Montpellier bila mafowadi Neymar na Angel di Maria walioingia ugani katika kipindi cha pili na kufunga mikwaju yao ya penalti.

PSG walikosa huduma za Mbappe wakati wa kupigwa kwa penalti kwa sababu aliondolewa uwanjani katika dakika ya 82 na nafasi yake kutwaliwa na Kean anayechezea mabingwa hao watetezi wa Ligue 1 kwa mkopo kutoka Everton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wachina wabadilisha mwelekeo na kufuatilia zaidi lugha za...

Hakimu atoa uamuzi wake kwa Kiswahili sanifu