• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Re Union yapiga moyo konde kujikaza kupanda ngazi

Re Union yapiga moyo konde kujikaza kupanda ngazi

JOHN KIMWERE, NAIROBI

MECHI za Kundi A kufukuzia taji la Nairobi West Regional League (NWRL) zinatazamiwa kushuhudia ushindani mkali muhula huu. Timu ya Re Union iliyopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Kaunti, ni miongini mwa vikosi 14 vinavyoshiriki kampeni za ngarambe hiyo.

Viongozi wa Re Union ambayo ni kati ya klabu kongwe hapa nchini wanasema kuwa, ingawa wanashiriki mechi za viwango vya chini wanajipatia miaka minne kuhakikisha wamefuzu kushiriki ligi kuu Kenya.

”Itakuwa furaha kubwa kwa wafuasi wetu endapo tutafaulu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu,” katibu wake, Caleb Ochieng Mumbo alisema na kutoa wito kwa wafadhili wajitokeze kuwapiga jeki kwenye juhudi za kupaisha soka la kikosi hicho.

”Kampeni za msimu huu bado sio mteremko lakini tunapania kujituma kiume kuhakikisha tunaibuka kileleni na kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili muhula ujao. Tunalenga kupambana mwanzo mwisho ili tutimize azma ya kufanya kweli kinyume na matarajio ya wengi.

Ingawa klabu hiyo imeanza kampeni zake vibaya, mwenyekiti wake, Charles Omollo Tude anasema wachezaji wake wanastahili kuzinduka ili kukabili wapinzani wao. ”Katika mpango mzima endapo tunahitaji kupanda ngazi msimu ujao lazima wachezaji wetu wajitolee kupiga shughuli bila kulegeza kamba,” mwenyekiti huyo alisema na kuongeza kwamba wachezaji wake hawana budi kufahamu kuwa hakuna kizuri hupatikana rahisi.

Kocha wake, Joseph Milimo anasema ”Kiasi wachezaji hawajarudi fomu vizuri baada ya kukawia kwa muda bila kushiriki mechi zozote kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.” Kocha huyo aliyewahi kufunza klabu za Ligi Kuu Kenya anasisitiza kuwa hali hiyo ilivuruga wachezaji wengi kimichezo.

USHINDI MMOJA

Ingawa wameshinda patashika moja kati ya mechi tano ambazo wameshiriki msimu huu anasema hawapo vibaya. Anatoa wito kwa wanasoka wake wazinduke maana wana kibarua kigumu mbele yao. Anataja baadhi ya wachezaji anaotegemea zaidi kwenye kampeni za muhula kama:Joseph Omondi (kipa), Michael Masaba, Brian Shikanga, Edwin Naze (mabeki), Erick Juma Shivaji, Oscar Ochieng na Dickson Gitae.

Kocha huyo anasema endapo watabahatika kupata ufadhili wana uwezo wa kujenga timu imara na kuirejesha katika hadhi iliyokuwa miaka iliyopita.

Re Union inajivunia kuibuka ya kwanza kubeba taji la Afrika Mashariki na Kati mara mbili mwaka 1976 na 1977. Kadhalika iliwahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu nchini mara mbili mwaka 1964 na 1975. Kulingana na historia ya klabu hiyo inastahili kuwa ikishiriki mechi za ligi kuu kama AFC Leopards na Gor Mahia kati ya zingine.

Klabu hiyo inajumuisha wachezaji kama:Joseph Omondi Ndekle, Nehemaa Omondi Ayieta, Paul Ojwang Wando, Fabian Omondi (makipa), Michael Masaba, Brian Shikanga, Brian Ochieng, Griffin Owino, Dancan Otieno na Edwin Naze(mabeki). Wengine wakiwa:Daniel Kimoli, Erick Juma Shivaji, Timothy Simiyu, George Ogaga, Caleb Maina, Yohana Machio, Meshark Godia, Dickson Gitae na Oscar Ochieng (viungo) nao washaambuliaji wakiwa:George Onyango na Khassid Ngoye.

You can share this post!

Luis Suarez afunga goli lake la 500 kitaaluma na kudumisha...

BACK TO BASIC FC yajivunia vipaji tegemeo