• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Real wakomoa Mallorca na kufungua mwanya wa alama 10 kileleni mwa jedwali la La Liga

Real wakomoa Mallorca na kufungua mwanya wa alama 10 kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walifungua mwanya wa alama 10 kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumatatu usiku baada ya kupepeta Mallorca 3-0 ugenini.

Baada ya kuambulia sare tasa katika kipindi cha kwanza, Vinicius Jr aliwaweka waajiri wake Real uongozini katika dakika ya 55 baada ya kushirikiana vilivyo na fowadi Karim Benzema.

Benzema aliyefungia Real mabao matatu katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) na kudengua miamba hao wa Ufaransa kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Machi 8, 2022 alipachika mabao mawili mengine ya waajiri wake dhidi ya Mallorca.

Alipachika wavuni mkwaju wa penalti katika dakika ya 77 kabla ya kufunga la tatu kupitia kichwa dakika tano baadaye. Matokeo yakiwa sare tasa, Mallorca nusura wafungiwe bao na Pablo Maffeo katika kipindi cha kwanza.

Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 66 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na nambari mbili Sevilla. Barcelona na mabingwa watetezi Atletico Madrid wanakamata nafasi za tatu kwa alama 51 mtawalia.

Real watakuwa wenyeji wa Barcelona mnamo Machi 20, 2022 katika gozi la El Clasico uwanjani Santiago Bernabeu.

Atletico watakaokuwa wageni wa Manchester United katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo Aprili 15, 2022 ugani Old Trafford baada ya kuambulia sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza nchini Uhispania, walitwaa taji la La Liga msimu uliopita wa 2020-21 kwa alama mbili zaidi kuliko Real.

Zinedine Zidane alijiuzulu mwishoni mwa msimu wa 2020-21 kabla ya Carlo Ancelotti kuondoka Everton na kurejea Real kwa awamu ya pili ikizingatiwa kwamba aliwahi kuhudumu kambini mwa miamba hao kati ya 2013-15.

Licha ya kushindia Real mataji ya UEFA na Kombe la Dunia katika awamu yake ya kwanza ya ukufunzi, Anceloti hakunyakulia kikosi hicho taji la La Liga. Sasa yuko pazuri zaidi kunyanyulia waajiri wake taji hilo kwa mara ya 35.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ada zisizo na maana zinachangia matokeo mabaya katika shule...

Serikali yaondolea wadhimini wa michezo ushuru

T L