• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Refa mpya kwa mechi ya Harambee Stars na Misri baada ya aliyefaa kupuliza kipenga kupata corona

Refa mpya kwa mechi ya Harambee Stars na Misri baada ya aliyefaa kupuliza kipenga kupata corona

Na GEOFFREY ANENE

REFA Thando Ndzandzeka kutoka Afrika Kusini atasimamia mechi ya kufa-kupona wa Harambee Stars dhidi ya Misri baada ya Victor Miguel de Freitas Gomes kupatikana na virusi vya corona.

Gomes, ambaye pia anatoka Afrika Kusini, ndiye alifaa kufanya majukumu hayo ya kupuliza kipenga katika mechi hiyo ya Kundi G ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2022 itakayosakatwa ugani Kasarani kuanzia saa moja usiku Machi 25.

Ndzandzeka, ambaye aliibuka refa bora wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini msimu 2015-2016, atasaidiwa na wanyanyuaji wa vibendera Zakhele Thusi Granville Siwela na Athenkosi Ndongeni naye Abongile Tom atakuwa afisa wa nne. Maafisa hao wanne ni raia wa Afrika Kusini.

Kamishna wa mechi ni Awuye Yusuf Suleiman kutoka Uganda. Mganda Dixon Adol Okello atasimamia usalama.

Mratibu mkuu ni Kelly Athanasie Mukandanga (Rwanda) naye Wycliffe Makanga kutoka Kenya ndiye afisa wa anayehusika na masuala ya janga la virusi vya corona. Maafisa hao wote wa kigeni waliwasili jijini Nairobi siku ya Jumanne.

Stars ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee itaelekea jijini Lome kukamilisha kampeni yake dhidi ya Togo mnamo Machi 29. Misri inaongoza kundi hili kwa alama nane ikifuatiwa na Comoros (nane), Kenya (tatu) na Togo inayoshikilia mkia kwa alama moja.

  • Tags

You can share this post!

Uturuki waduwaza miamba Uholanzi kwa kichapo cha 4-2

Harambee Stars ilipiga Misri mara ya mwisho miaka 44...